*BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA. Yer 17:5 SUV*

Kila mtu anaweza akawa na nafasi ya kujivunia wazazi wake, watoto wake, ndugu zake, marafiki zake, vile wanavyomsaidia mahitaji mbalimbali katika maisha yake. Kujivunia huku kunaweza kusiwe na tatizo lolote ikiwa mtu huyu hatawaona ni watu wa muhimu sana na kuondoa nafasi ya Mungu.

Wapo watu wamejitafutia laana wenyewe kwa kuondoa nafasi ya Mungu kwenye mioyo yao na kuwafanya watu wao ndio kila kitu kwenye maisha yao, mtu anamwona mzazi wake ndio kila kitu, mtu anamwona mtoto wake ndio kila kitu kwake hakuna chochote nje na mtoto wake.

Wengine wanawaona waume zao au wake zao ndio kila kitu kwao, hata ukimwambia habari za Mungu hana mpango huo maana anajua chochote akikihitaji atakipata kwa mume/mke wake. Hii dhana imejengeka kwenye ufahamu wake hivyo na kuona anaishi vizuri kwa sababu ya mke/mume wake.

Kuondoa nafasi ya Mungu kwa watu sio jambo gumu na lisilowezekana, unaweza usijue sana kama umeondoa nafasi ya Mungu kwenye moyo wako ila matendo yako na vile unajifahamu unaona kabisa matumaini yako na mategemeo yako makubwa yamehamia kwa mtu.

Wengine wanashindwa kuhimili wanapoondokewa na wale waliowategemea asilimia mia moja, utashangaa aliyemtegemea anakufa leo baada ya siku chache na yeye anafariki, unashindwa kuelewa nini kimetokea. Wengine hawafi ila anarukwa na akili zake, unashangaa ghafla mtu anakuwa kichaa.

Hiyo ni kwa upande wa mtu ambaye ameondoa nafasi ya Mungu na kumweka mwanadamu mwenzake na kumwona kila kitu kwake, wengine huwa hawafichi hisia zao husema kabisa wewe ndio kila kitu kwangu bila wewe siwezi ishi. Wengine wanaenda mbali zaidi na kusema wewe ni roho yangu, na kweli unaona nafasi ya Mungu haipo tena moyoni mwake.

Zipo faida za kumtegemea Mungu, kumwona Mungu ndio kila kitu kwako, hata kama unawapenda wazazi wako, watoto wako, mume wako, mke wako, ndugu zako au marafiki zako, lakini hawachukui nafasi ya Mungu. Wanabaki katika nafasi zao ila nafasi kubwa moyoni mwako na tegemeo lako kubwa ni kwa Mungu wako aliye hai.

*Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda. Yer 17:7-‬8 SUV*

Mtu anayemtegemea Mungu asilimia mia moja hana hofu, na ana kinga ya kutosha, wapo watu wanakuwa na hofu kubwa ya maisha kwa sababu wale waliowategemea wamekumbwa na matatizo au wamefilisika, wanakuwa wanaona mwisho wa maisha yao umefika.

Wengine wanakuwa na hofu wataishije maana wale waliowategemea wamewakimbia, hii yote ni kwa sababu waliondoa matumaini yao kwa Mungu. Lakini mtu ambaye anamtegemea Mungu hata inapotokea tatizo utamwona ana tofauti kubwa sana na yule aliyemtegemea mwanadamu mwenzake.

Sisi kama wana wa MUNGU tunapaswa kuweka matumaini yetu mbele za Mungu, mioyoni mwetu panaswa kuwa na nafasi kubwa ya MUNGU. Hata inapotokea changamoto yeyote tuone wa kutusaidia katika changamoto hiyo ni Mungu na sio mjomba wala mama, hapa tutakuwa tumeishinda hofu. Anapotokea mtu ametusaidia tumtukuze YESU na kumrudishia sifa na utukufu, tuone Mungu mwenyewe ametusaidia ila ametumia mtu.

Tuache kuweka matumaini yetu kwa watu tutamkosea Mungu bure, tuweke matumaini yetu kwa Yesu Kristo, chochote tuone yeye atatusaidia, hata kama tunaona mvua ni changamoto mioyo yetu imtumaini yeye. Hata kama tunaona kuna vitu vinapanda gharama kubwa, tusiweke matumaini kwa mtu na kumwona yeye ndio atatusaidia, acha Mungu mwenyewe aseme na mtu.

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081