Wakati wenzako wanalia, wanamwona fulani ndiye chanzo cha matatizo yao, wanaona isingekuwa fulani wasingefika hapo walipo. Wakati wengine wanaona hivyo, yupo mtu anaona kwa tofauti kabisa.

Hata kama wamezungukwa na tabu nyingi kila kona, kuna kitu cha tofauti wanakiona katika tabu zao, ipo fursa wanaiona na wapo tayari kuitumia hiyo nafasi.

Wanaweza wakawa washauri wa wenzao waliopo kwenye shida moja, au waliopo kwenye mateso ya pamoja, wakati wenzao wanaongea maneno mabaya juu ya watu fulani. Wale wanaoona kwa jicho la tofauti, wanakuwa na maneno mazuri ya kuwasihi wengine wasiongee hovyo.

Hili tunajifunza kwa wahalifu wawili waliounganishwa na Yesu Kristo kwa ajili ya kusulubiwa, mhalifu mmoja alianza kumtolea Yesu Kristo maneno ya kejeli. Lakini mhalifu mwingine wa pili alikuwa anamwona Yesu Kristo hana hatia yeyote na hukustahili kufanyiwa kama wao.

Rejea: Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. LK. 23:39‭-‬43 SUV.

Haleluya, sijui kama umesoma vizuri hiyo mistari niliyokushirikisha hapo juu, kama umesoma kwa haraka unaweza kurudia kusoma tena kwa umakini. Utajifunza kitu kikubwa sana hapo kati ya wahalifu hao wawili, wakati mwingine anaendeleza maneno ya kejeli kwa Yesu Kristo, mwenzake alimwona Yesu kwa namna ya pekee sana.

Tena yule wa pili akamkemea kwa kumwambia hivi; Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? LK. 23:40 SUV.

Huyu mhalifu wa pili naona akili zake zilikuwa zimetiwa nuru ya kimbingu kabisa, ilikuwa ni ngumu sana kumwona Yesu Kristo kama mtu mwema, mtu asiye na hatia, katikati ya mateso makali.

Tena kinachofurahisha zaidi ni pale alipomwambia Yesu Kristo amkumbuke atakapoingia katika ufalme wake, usisahau haya mazungumzo yote yalikuwa yanafanyika wakati wote wapo msalabani, wapo kwenye maumivu makali, kila mmoja anapambana na mauti.

Na kweli Yesu Kristo alimjibu pale pale kwa kumwambia hivi; Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. LK. 23:43 SUV.

Jamaa huyu aliona fursa, na akapata tiketi ya kuingia peponi moja kwa moja, na mwenzake aliishia jehanamu. Unaweza kuona jinsi gani mazingira hayawezi kumzuia mtu asifike mbinguni, kama huyu mhalifu wa pili alifanya mapatano mapema na Yesu Kristo na akapata kibali cha kuingia peponi. Hata kwa mwenzake ilikuwa inawezekana kabisa sema alikuwa amevaa roho ya chuki dhidi ya Yesu Kristo kama ilivyo leo kwa wengi.

Hebu kuwa makini hasa pale mnapojikuta mpo kwenye wakati mgumu, usiishie kulalamika, angalia kipi cha kufanya wakati huo, epuka maneno ya kejeli kama ya mhalifu wa kwanza. Jifunze kwa mhalifu wa pili, mhalifu aliyebadili uelekeo na kupata nafasi ya kuingia peponi moja kwa moja pamoja na Yesu Kristo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com