“Nikioa/nikiolewa nitabadilika na kuacha hii tabia mbaya ya kutembea na wanawake/wanaume hovyo.”
Moja ya kauli ambayo vijana wengi huwa wanajisemea ni hii kauli, kauli ambayo huwa inawapa uhalali wa kuendelea kufanya uasherati bila kuwa na wasiwasi wowote huku wakijifariji kuwa siku wakioa/wakiolewa wataacha hiyo tabia uasherati.
Uasherati ukimkamata mtu huwa huangalii kama ameoa au ameolewa, mtu huyo asipolitatua hilo tatizo kabla ya ndoa alafu akawa ameingia nalo, uwe na uhakika ataendelea nalo.
Ukweli ni kwamba tabia ya uasherati/uzinzi haiondolewi na mtu kuoa/kuolewa, ikiwa mtu mwenyewe atashindwa kujirekebisha kabla ya ndoa kuna uwezekano mkubwa kuendelea na hiyo tabia akiwa ndani ya ndoa.
Watu walioingia kwenye ndoa wakiwa hawajaweza kuacha hiyo tabia, wamejikuta wakiendeleza michezo yao wakiwa ndani ya ndoa. Hii imesababisha ugomvi kwenye ndoa na wengine kusambaratisha ndoa zao kwa sababu ya hii tabia uasherati.
Ukiwa na tatizo hili la kutembea na wanaume/wanawake, yaani kila mwanamke/mwanaume anayekuja mbele yako unataka ulale naye, hakikisha unalitibu kwanza, unaweza kuona kama ni ngumu ila unapaswa kufanya hivyo.
Huwezi kulitibu kwa akili zako, unamhitaji Yesu Kristo, mruhusu Yesu ndani yako, unaweza kuwa unaenda kanisani kila siku ila Yesu hayupo ndani yako. Yesu akiwa ndani yako hofu ya Mungu itakuwa ndani yako, uhusiano wako ukiwa mzuri na Mungu hutaweza kufanya dhambi kwa ujasiri wowote.
Usipolitibu hilo tatizo linalokukabili ndani yako, usipodhamiria kuliacha na kutubu, ukaenda nalo hivyo hivyo utaleta shida kwenye ndoa yako, utamwona mke/mume wako hakutoshi utahitaji kuendelea na wengine wa nje.
Mbaya zaidi wengine huwa wanaendelea na wanaume/wanawake wale waliokuwa nao kabla ya ndoa, ndio maana utakuta mwanandoa hataki mwenzake ashike simu yake. Kwanini hataki, anajua muda wowote ujumbe unaweza kuingia wa mwanaume/mwanamke mwingine, au kuna jumbe ambazo hataki zisomwe na mwenzake.
Utasema hilo sio kweli kuna watu walikuwa na tabia hizo ila walipoingia kwenye ndoa wakawa watu wazuri, nikuambie ukipata muda wa kuongea nao watakueleza mambo mazito. Ukiona hivyo ujue walikutana na Yesu na kuona wanachokifanya hakifai na kuamua kuacha, lakini walishakutana na changamoto nyingi kwenye ndoa zao.
Ukiwa kijana na bado hujaoa/hujaolewa hupaswi kuingia kwenye ndoa ukiwa na hiyo tabia, amua ndani ya moyo wako kuacha kabisa kisha tubu mbele za Mungu. Mruhusu Roho Mtakatifu awe kiongozi wa maisha yako, baada ya hapo oa/olewa ukiwa tayari umepona shida iliyokuwepo ndani yako.
Ukisema haina shida, ukawa na mchumba ambaye unategemea kuishi naye siku za usoni alafu unaendelea na michezo yako michafu na wanawake/wanaume wengine. Ukifanikiwa kuingia naye kwenye ndoa, hako kamchezo utaendelea naye na mume/mke wako akiwa ndani.
Nirudie tena tabia mbaya ya uasherati ikiwa ndani yako kijana haitaondolewa na kuoa/kuolewa kwako, hakikisha unaiacha kwanza ndipo uingie kwenye ndoa. Tena ukiacha hiyo tabia macho yako ya ndani yatakuwa na uwezo wa kuona vizuri na Mungu atakuwa pamoja na wewe.
Usiwe wa vuguvugu, uwe wa moto(UFU. 3:15), Mungu atakutetea sana kwenye maisha yako ya wokovu, changamoto ni nyingi ila utazishinda ukiwa kwa Yesu, na ukiwa unaongozwa na Roho Mtakatifu.
Usiache kutembelea mtandao wetu www.chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi na unaweza kujiunga nasi kwa kuweka email yako uwe unapokea masomo moja kwa moja kwenye email yako. Pia tunakukaribisha kusoma biblia kila siku na kushirikishana yale tuliyojifunza kwa njia ya wasap, wasiliana nasi kwa wasap +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081