Injili ya kweli ni yale maisha halisi anayoyaishi mtumishi wa Mungu, inakuwa injili feki pale unapomwambia mtu acha dhambi. Wakati wewe mwenyewe ile ile dhambi unayoikemea, wewe mwenyewe unaifanya hiyo dhambi.

Utakuwa mwongo, kama unamwambia mwenzako kwa Yesu Kristo raha, wakati wewe mwenyewe huoni hiyo raha. Maisha yako yamejaa dhambi chungu nzima.

Tabia hii imeshamiri sana kwa wakristo wengi, maisha yetu hayafanani na maneno tunayozungumza. Mtu anakwambia Yesu anaweza mambo yote, yule yule mtu unamkuta anaenda kwa waganga wa kienyeji.

Mtu anakwambia acha kunywa pombe ni mbaya, alafu unamkuta yeye mwenyewe anakunywa kwa siri. Anakuwa hana tofauti na aliyekuwa anamkemea kuhusu pombe.

Mtu anakwambia na kukusisitiza soma Neno la Mungu ni zuri sana, alafu yeye mwenyewe hasomi kabisa. Na uwezakano wa yeye kusoma upo ila anakuwa hasomi.

Mtu anakwambia acha uzinzi/uasherati, anakuwa mkali kweli kweli, na kama ana nafasi kanisani anaweza kukutenga kabisa. Huyo anayekuambia hivyo, anatembea ovyo na wanaume/wanawake wengine.

Mtu anakwambia acha wizi ni mbaya, alafu huyo huyo anayekuambia hivyo, ni mwizi namba moja, anayeibia watu kwa siri.

Unapompelekea mtu habari za Yesu Kristo, alafu wewe mwenyewe ukawa unahitaji kupelekewa hiyo injili. Inakuwa sio kabisa, haijalishi wewe ni mtumishi, kama unahubiri watu waache dhambi waje kwa Yesu Kristo.

Alafu wewe mwenyewe mtumishi ukawa unazitenda dhambi zile zile, huna unachokifanya, wewe mwenyewe unahitaji kukombolewa na Yesu Kristo.

Huwezi kuwaambia watu iweni waaminifu, alafu wewe mwenyewe sio mwaminifu, unawatendea wengine mabaya. Una madeni chungu nzima, ukiambiwa ulipe unakuwa unawadanganya na kuwazungusha wale wanaokudai, mpaka wengine wameacha kukudai.

Usijipe maksi ya kusema upo safi, wakati yale yale wanayoyafanya wengine wawe wachafu. Wewe ndiye kinara wa kuyafanya hayo, ipo tofauti gani kati yako na yule unayetaka kumsaidia?

Sawa na daktari anakwambia sigara ni hatari kwa afya yako, tena anakwambia inaharibu mapafu, achana nayo kabisa. Anakusisitiza uache kuvuta sigara, alafu yeye mwenyewe ni mvutaji mzuri kabisa wa sigara.

Hii ni mbaya sana mbele za Mungu, mtu anayemwambia mwenzake acha uzinzi, alafu yeye mwenyewe ni mzinzi haswa. Hata kama watu wengi hawajui kutokana na kufanya mambo yake kwa siri kubwa, Mtu anakuwa hana tofauti yeyote na anayemwambia.

Hili tunajifunza kupitia andiko hili takatifu, linasema hivi;

Rejea: Je! Naweza kuwa safi nami nina mizani ya udhalimu, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu? Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao. MIK. 6:11‭-‬12 SUV.

Mizani ya udhalimu tunaifananisha na maisha ya mkristo yasiyofaa, maisha ambayo watu wa duniani wasiomjua Kristo wanayo. Na yeye yale maisha anakuwa nayo mkristo huyu anayejiita yeye ni msafi.

Kama wewe ni muongo na mwingine akawa mwizi, huwezi kusema wewe upo safi, alafu yule mwenzako mwizi hayupo safi.

Kama wewe ni daktari unatoa mimba za wadada, usijione wewe upo safi, alafu yule aliyetoa mimba yake si safi. Unapaswa kuelewa wote ni wachafu mbele za Mungu.

Tunapaswa kujichunguza sana, maisha yetu ya wokovu, yanapaswa kuwa barua njema. Kile unakihubiri kiwe ndio unakiishi, usiwe unakazana kuwaambia watoto wako acheni jambo fulani baya. Alafu wewe mwenyewe unayafanya yaliyo mabaya zaidi.

Yesu anakupenda, badilika sasa.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.