Kila mmoja ana utambulisho wake kwa watu, watu wanaposikia fulani moja kwa moja wanapata picha yako. Matendo yako ndiyo yanakufanya utambulike, wengine maumbile yao, vyovyote vile watu wanakuwa wanakutambua kwa vile ulivyo.

Kuna watu wanatambulika kwa kugombanisha watu kwa maneno, hawa wanakuwa na sifa hii mbaya. Ukiwataja tu kwenye masikio ya watu wanapata picha ya fulani.

Wapo watu wanafahamika kwa utapeli, yaani mtu anakuwa na maneno mazuri wakati anakuja kukuomba msaada wa fedha. Lakini moyoni mwake anajua hatakurudishia, akishapewa ndio moja kwa moja hatairudisha hiyo fedha.

Wapo watu wanafahamika kwa uaminifu wao, ukimtuma kitu atakileta kama kilivyo, kama ulimpa fedha ya kutosha na akakuta pungufu ya hapo. Ujue kiasi kitachozidi atakirudisha.

Wengine wanajulikana kwa kukarimu wageni, ukisikia mama fulani moja kwa moja unapata picha ya huyo mama. Sifa yake ya kupokea watu vizuri inakuwa inaishi ndani ya mioyo ya watu.

Yupo mwalimu anajulikana kwa sifa ya kuchapa sana wanafunzi, sifa yake kubwa sio kufundisha vizuri, yeye sifa yake kubwa ni kupiga wanafunzi. Kwa hiyo unapomuuliza mtoto kuhusu mwalimu fulani moja kwa moja atataja sifa ya mwalimu huyo.

Kumbe Matendo yetu ndio yanatutambulisha zaidi kuliko vile tunavyoweza kuwalaghai watu kwa kuvaa uhusika fulani usio wetu. Vile unaishi, vile unatenda, vile unafanya, ndivyo watu wanavyoweza kukufahamu.

Kama unafundisha vizuri sana Neno la Mungu, na Mungu anakutumia ipasavyo, na wewe unajibidiisha sana kwa mambo ya Mungu. Watu watakujua kwa hayo unayotenda.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu Kristo wakati anawauliza wanafunzi wake, alitaka kujua watu wanamtambuaje, wanamfahamu yeye kama nani, wanamsemaje huko nje. Hilo swali lake lilimpa majibu mengi sana, hebu tutazame maandiko matakatifu;

Rejea: Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. MT. 16:13‭-‬14 SUV.

Unaona hapo, wapo walimwona ni Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia. Kwanini walimwona Yesu Kristo ni miongoni mwa watu hawa waliosemwa hapo, hawa watu walikuwa wanawafahamu hawa watumishi wa Mungu.

Utendaji kazi wa Yohana, Eliya, Yeremia, asilimia kubwa ulifanana sana na utendaji kazi wa Yesu Kristo. Sasa hawa watu walishindwa kuelewa ni nani huyu.

Hata wewe ndugu yangu, Yesu Kristo akiwa ndani yako sawa sawa, matendo yako yatafanana na tabia ya Yesu Kristo. Tabia ya watu waliokoka sawasawa asilimia kubwa zinafanana Duniani kote, maana Yesu ni yule yule.

Sijui watu wanakutambua kwa sifa ipi, sifa njema, ama sifa mbaya, una uwezo wa kurekebisha hilo na ukawa na sifa njema. Kama watu wanakunena kwa mabaya na unasema umeokoka na hayo yanayonenwa ni kweli, unapaswa kujirudi kwa upya mbele za Mungu.

Tambulika kama mtu uliye na Yesu Kristo ndani yako, mtu usiye na kona kona za hovyo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com