
Tumekuwa tukijiuliza hili sana, kwanini lile usilolipenda kulifanya ndilo tunajikuta tunalifanya, na lile tunalolipenda ndilo hatulitendi kabisa.
Mtu hapendi uzinzi/uasherati ila anajikuta anafanya na bado anaingia kanisani, hapendi kufanya hivyo ila anajikuta amefanya.
Mtu hapendi pombe ila kila akijaribu kuacha pombe anajikuta anainywa sana, tena wakati alipumzika kidogo siku akizidiwa kidogo anajikuta ameinywa zaidi ya siku nyingine.
Mtu hapendi tabia fulani mbaya kwake, kila akijaribu kuacha hiyo tabia anajikuta anaifanya.
Jibu la hili jambo limepatikana, hakuna kingine ndani yako zaidi ya dhambi itendayo kazi ndani yako, hicho tu ndio kinakufanya uendelee kufanya yasiyompendeza Mungu.
Rejea: Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. RUM. 7:20 SUV.
Dawa ya kumaliza hilo tatizo lako ni kuruhusu Yesu Kristo aingie sawasawa ndani ya moyo wako, yaani uamue kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Bila hivyo utaendelea kuteswa na hiyo tabia chafu ndani yako, tabia ambayo hupendi kuifanya ila unaona inaendelea kukusakama ndani ya maisha yako.
Jitoe kwa Yesu Kristo leo, ili uvifishe viungo vyako vinavyotamani kumtenda Mungu dhambi.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com