Mahali popote pale mara nyingi huwa kuna kanuni/taratibu zake, ukikuta sehemu hakuna taratibu. Hiyo sehemu itakuwa sio salama sana, hata kama inaonekana ni sehemu salama sana kwako.

Familia imara na inayoenda katika maadili mazuri, lazima familia hiyo itakuwa ina utaratibu mzuri ambao wamejiwekea na kufuata. Wazazi watakubaliana nami kuhusu hili, ukikuta watoto wa familia fulani wana maadili mazuri. Uwe na uhakika wazazi wa watoto wale wamewalea katika utaratibu fulani uliowapika vizuri mpaka wakawa watoto wazuri.

Huwezi kukuta watoto wana maadili mazuri bila wazazi/walezi wao kuhusika katika malezi hayo. Na malezi mazuri hayawezi kutokea tu ghafla, lazima kanuni zilizowekwa zilikuwa zinafuatwa ndipo zikazaa matunda ya kijana, mama, baba mzuri mwenye maadili mazuri.

Fuatilia hata zile shule zinazosimamia kanuni walizojiwekea, shule hizo zinakuwa na kiwango kikubwa sana cha kuzalisha wanafunzi wenye kiwango kizuri cha elimu. Maana kanuni walizojiwekea hadi mwalimu anapaswa kuzitii na kuzifuata, ukienda kinyume cha hapo zipo hatua za kinidhamu zitakuchukuliwa dhidi yake.

Unaweza kuona ni jinsi gani taratibu/kanuni zilivyo na mchango mkubwa sana katika maisha ya mwanadamu. Kanuni zinaweza kumwongoza mtu kwenye njia sahihi, vile vile kanuni zinaweza kumfanya mtu akawa na maadili mabaya. Inategemeana na hizo kanuni zikoje mahali zinamwongoza.

Pia kunaweza kukawa na kanuni/taratibu nzuri ila kukawa hakuna mkazo wa kuzingatia hizo kanuni. Uwe na uhakika hizo kanuni hazitakuwa na msaada wowote, kanuni zinaleta maana pale kiongozi wa kundi husika atapokuwa na mkazo wa kuzingatia kanuni.

Wengi wetu tumefikiri tukiokoka hatupaswi kuwa na kanuni, wengi wameona kwenda kwa uhuru bila kujiweka utaratibu wowote ni nzuri kwao. Badala yake wamejikuta wakiangukia pabaya, maana ukiwa kama mkristo unapaswa kujiwekea utaratibu mzuri wa maisha yako.

Mungu wetu ni wa utaratibu ndivyo Neno lake linavyotuambia, huwezi kuwa msomaji wa Neno la Mungu bila kulijua hili. Kama unasoma Neno la Mungu alafu huna utaratibu wowote, ni mtu wa kuona kila kitu ni sawa kwako, unapaswa kujitathimini upya.

Rejea: Naye mkuu atakapoingia, ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango lile, naye atatoka kwa njia iyo hiyo. Lakini watu wa nchi watakapokuja mbele za BWANA katika sikukuu zilizoamriwa, yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kaskazini ili kuabudu, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kusini; na yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kusini, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kaskazini; hatarudi kwa njia ya lango aliloingia kwalo, lakini atatoka kwa kwenda mbele moja kwa moja. Naye mkuu atakapoingia, ataingia katikati yao, nao, watakapotoka, watatoka wote pamoja. EZE. 46:8‭-‬10 SUV.

Haya yalikuwa ni maelekezo ya namna ya kuingia hekaluni, Mungu alikuwa anampa utaratibu mtumishi wake Ezekiel. Utaratibu huu ulipaswa kuzingatiwa sana kwa kila mmoja wao, wakati wa kuingia na wakati wa kutoka, walipaswa kujua wanaingilia wapi na wanatokea wapi baada ya kumaliza ibada.

Na mahali pa kuhani alipaswa kwenda kuhani tu, na angejaribu kwenda mtu mwingine nje na utaratibu uliowekwa. Ilikuwa lazima mtu yule apate madhara makubwa.

Bila utaratibu hatuwezi kufanya vitu vikaeleweka sana, bila utaratibu hatuwezi tukaongea tukaelewana. Lazima pawepo na kuachiana zamu, akiongea huyu akamaliza, anaongea na mwingine ili pawepo kusikilizana.

Ibada zetu zina utaratibu wake, tunapaswa kutunza utaratibu wetu mzuri ambao unatufanya kila mmoja awe na nidhamu mbele za Mungu. Hatuwezi kwenda ilimradi tunaenda lazima tufuate utaratibu uliowekwa na kanisa.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.