Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, jina lipitalo majina yote chini ya jua, habari za wakati huu ndugu yangu katika Kristo, bila shaka unaendelea kumwamini Mungu na kumtegemea katika maisha yako yote.
Leo napenda kukushirikisha hili jambo la msingi sana, ili unapodai haki zako mbele za Mungu uwe na ujasiri ulioambatana na hoja za msingi. Unapomwambia Mungu naomba kitu fulani uwe na uhakika utakipata kwa sababu alisema uombe.
Wakati mwingine tumeomba kwa mashaka, tukiwa hatuna imani iliyojaa viwango vizuri kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe tunalomwomba. Hii inaweza kusabishwa na mazingira, na jinsi watu wengine wanavyolitazama hilo jambo kibinadamu.
Tunapomwelewa Mungu vizuri na tukawa na uhusiano mzuri na yeye, hakuna kitu chochote kitaweza kututisha na kutuogopesha. Nakwambia kweli, usipoamini ni wewe umeamua kutokuamini.
Alichokiahidi Mungu kwetu ni kweli wala hajabahatisha, wala hajatuahidi kwa bahati mbaya. Anaposema Yesu alichukua mateso yetu, tujue ni kweli, anaposema yeye ni kimbilio na msaada wa kweli, tujue ni kweli. Tujenge twasira hiyohiyo kuwa tukiwa ndani ya Yesu na Yesu ndani yetu, tuwe na uhakika wa maisha yetu.
Unapoelewa baba yako ndio anapaswa kukupa kalamu na madaftari ya shule, huna haja kuwa na mashaka tena, ya kujiuliza utapata wapi daftari na kalamu ya kuandikia. Akili zako zote zinakupeleka moja kwa moja kwa mzazi wako, huwezi kwenda kwa jirani kuomba pesa ya kununua kalamu wakati mzazi wako yupo, na anauwezo wa kukusaidia.
Hebu jifunze sana hili, kwenda mbele za Mungu kwa mashaka mashaka ya kupata au kukosa, hiyo ni imani mbaya ya mtoto asiye na uhusiano mzuri na mzazi wake. Mtoto mzuri anayesikiliza wazazi wake, hawezi kwenda kuomba kitu kwa wazazi wake kwa hofu.
Kwanini unateswa na dhambi ya uzinzi/uasherati wakati Mungu amekataza na anakutaka uishi maisha Matakatifu. Kwanini unapata wasiwasi wa kupata mume/mke mwema ambaye Mungu mwenyewe amepanga uishi naye. Hii ni ishara kwamba hujui ahadi ya Mungu juu ya maisha yako.
Mungu akisema utabarikiwa mpaka uzao wako wa nne, amini itakuwa hivyo, Mungu akisema ukinitumikia katika roho na kweli, atakuheshimisha, amini hivyo. Siku ikitokea unaona mambo yanaenda ndivyo sivyo, mkumbushe ahadi yake kwako.
Haya ninayokuambia sio hadithi, nakueleza vitu halisi kutoka ndani ya Neno la Mungu, ambapo mfalme Suleiman anayathibitisha haya.
REJEA: Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi. 2 NYA. 6:16-17 SUV.
Tumebaki kama watoto wasio na baba yao, kwa sababu ya kunyamaza kimya huku tukifikiri hakuna anayeweza kutusaidia hitaji letu. Mungu huyuhuyu aliyetuumba na aliyetujua hata kabla ya kuzaliwa kwetu, ndiye huyuhuyu anayejua mwanzo wetu na mwisho wetu.
Mungu amekuambia fuata hili ukalifuata, ukafika wakati unahitaji kitu kutoka kwake, mweleze, usikae kimya ukifikiri atakufanyia tu. Yeye anasema ombeni nanyi mtapewa, ikiwa hatujaomba, ina maanisha sio wahitaji, hata kama kipo tunachokihitaji.
Kuanzia sasa mwone Mungu kwa sura ya tofauti, anza kuona maandiko unayosoma katika biblia sio stori za mawe yalikuwaga nyama, au sio mtu alitokana na nyani hapo zamani. Mweleze Mungu ulisema hivi na hivi kupitia Neno lako, naomba unipatie, naomba unisaidie, naomba uwe kiongozi wangu, naomba unitoe katika mateso ya ndoa yangu, naomba uniondolee matatizo haya na haya kazini kwangu.
Hayo ni maombi ya mtoto anayejua haki zake kwa mzazi wake, anapeleka hoja za msingi, na sio kulialia bila kueleza anataka nini kwa baba yake.
Naamini mpaka hapa umepata kitu cha kukusaidia katika maisha ya kiroho na kimwili, endelea kujifunza NENO la MUNGU zaidi, upate kujua haki zako za msingi.
Nikushukuru sana kwa muda wako, endelea kutafakari uweza wa MUNGU juu ya maisha yako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com