Zipo taarifa ambazo zilifika kwa walengwa, na taarifa hizo zikaleta hasara kubwa katika maisha yao. Wapo wengine walipata matatizo ya kiafya baada ya kupokea taarifa nzito na wakashindwa kuhimili maumivu yao.

Huwezi kuzuia kwa asilimia zote kutopata taarifa mbaya, utakataa kupokea taarifa kwa kuweka kizuizi cha wewe kutokupokea taarifa ya aina yeyote ile mbaya. Bado utapokea kwa namna usiyoitarajia utajikuta umeipata. Pamoja na hayo yote,  bado unayo sababu ya kuwa makini sana na taarifa unazopewa/unazoletewa.

Taarifa zinaweza kukuvuruga kiasi kwamba ukija kushtuka utakuwa umeharibu mambo yako mengi sana. Usisubiri uharibikiwe, unapaswa kuwa na maarifa ya kukusaidia kuepukana na hilo.

Shetani anaweza kutumia taarifa mbaya  kukuumiza, zinaweza zikawa taarifa za misiba, taarifa mbaya za kazini kwako, taarifa mbaya zinazohusu biashara yako, na taarifa mbaya juu ya huduma yako.

Taarifa hizo unazoletewa zinaweza zikawa na ukweli  ila sio vile zinaelezwa kwa uzito mkubwa, unaweza ukaletewa taarifa ya watoto wako wote wamekufa. Lakini katika uhalisia wenyewe aliyekufa ni mmoja tu.

Hili tunaliona kwa mfalme Daudi, aliletewa taarifa mbaya, taarifa ambayo ninaweza kusema leo kuwa ilikuwa imekolezewa chumvi. Ule ukweli wake uliongezewa chumvi kiasi kwamba ikawa tofauti.

Rejea: Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. 2 SAM. 13:30 SUV.

Unaona hapo, aliyeuwawa alikuwa Amnoni ila ikatengenezwa kuwa watoto wote wa mfalme walikuwa wameuwawa. Hii ni taarifa mbaya sana iliyojaa uongo ndani yake.

Unaweza kuona ni hadithi fulani hivi, Yesu akufungue macho uweze kuelewa, maana haya mambo yanatokea sana katika maisha yetu. Mungu akusaidie katika hili, taarifa mbaya zinaweza kukupoteza kabisa, Yesu asipoingilia kati.

Baadaye moja ya mtumishi wake aligundua jambo, akawa amempelekea taarifa sahihi, na kumwondolea ile taarifa ya kwanza ya kuawawa watoto wake wote.

Rejea: Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. 2 SAM. 13:33 SUV.

Hadi upate usahihi wa taarifa uliyoletewa, huenda ukakutwa una hali mbaya sana, ukakutwa umeumia sana, ama umelia sana. Ndio maana ni muhimu sana kutopokea kila taarifa na kuiweka moyoni mwako.

Taarifa zingine unapaswa kuzifanyia uchunguzi wa kina, itakusaidia sana, wakati mwingine taarifa zingine zinaweza kutusukuma kufanya maamuzi mabaya. Alafu hayo maamuzi yakaja kuwa majuto katika maisha yetu.

Mungu atusaidie sana.
👉Usiache kusoma neno la Mungu.
👉Usiache kuomba Mungu kwa bidii.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81