Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo, Mungu wetu ni mwema sana ametupa nafasi nyingine tena ya kuendelea kujifunza Neno lake takatifu.

Leo tunajifunza wema wa Mungu kupitia kwa Elihu akimweleza mtumishi wa Mungu Ayubu, jinsi ulivyo ukuu na uweza wake Mungu kwetu Wanadamu.

Kuna mengi ya kujifunza, hasa ukizingatia Ayubu akiwa anapitia katika majaribu mazito. Pamoja na kupita huko katika majaribu, Mungu alikaa kimya kiasi kwamba unaweza kusema Ayubu hakuwa na mahusiano mazuri na Mungu.

Tukiwa tunasoma maandiko matakatifu, tunazidi kuona jinsi tunavyoishi maisha yetu ya wokovu. Tunaweza kukutana na changamoto mbalimbali ngumu zingine zikiwa na lengo za kutupima imani yetu juu ya Mungu, na zingine zikiwa na nia za kutupoteza kabisa kwenye njia sahihi ya wokovu.

Tunaweza kujifunza mambo yafuatayo juu ya Mungu wetu, fuatana nami;

1. Mungu hamdharau mtu.

Mungu wetu anampenda kila mtu, ni sisi wenyewe huwa tunafika wakati tunajidharau wenyewe na tunamwacha wenyewe. Wakati mwingine ni kutojua wema wa Mungu kwetu, kwa sababu ya kukosa ule uhusiano wake wa karibu kupitia Neno lake.

Unaweza kuona ndani yako umeanza kuwa na dharau kwa watu wengine, unapoona hiyo hali ujue Roho Mtakatifu hayumo ndani yako. Kwa sababu moja ya tunda la Roho ni upendo.

Sifa ya Mungu moja wapo ni hamdharau mtu wake, ikiwa ni hivyo, na wewe umempokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako. Je inakuwaje roho ya dharau inakuwa ndani yako? Ina maana moja kwa moja ipo shida ndani yako. Ambayo unapaswa kuishughulikia mapema.

Rejea; Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu. Ayubu 36 :5 SUV.

2. Mungu huwapa/huwarejesha tena haki zao walionewa.

Wapo watu waovu na wanaendelea kutenda maovu, hata pale wanapoonywa huwa hawasikii. Wakati mwingine huwatendea mabaya wengine wasio na hatia yeyote.

Unakuta watoto wanapoteza wazazi wao, ndugu wanatumia nafasi ile kuwanyang’anya mali zao za urithi wa wazazi wao. Unakuta mama mjane ameachwa na mume wake, ndugu wanatumia nafasi ile ya kuondokewa na mume wake, kumfukuza nyumba walioishi na mume wake miaka yote.

Mungu atazamapo manyanyaso hayo kwa watu wake wamchao katika roho na kweli, uwe na uhakika Mungu atarejeshe kile kilichoibiwa na adui.

Ndio maana wale matajiri wengi wenye mali za uzalimu hufa vibaya, ndio maana wale waliopata fedha kwa njia zisizo halali. Mwisho wao huwa mbaya sana, maana zingine ni laana.

Rejea; Hauhifadhi uhai wa waovu; Lakini huwapa wateswao haki yao. Ayubu 36 :6.

3. Mungu haachi kuwatazama na kuwapigania wale wamchao.

Upo wakati mgumu tunaweza kupitia alafu tukashangaa tumewezaje kuvuka hilo eneo. Maana unakuta kwa jinsi ulivyokuwa unaona kwa akili za kibinadamu, uliona umefika mwisho wako wa kufikiri namna ya kutoka kwenye shida iliyokukabili. Ila Mungu huwa haachi kututazama wana wake, kwa macho yake kututoa pale tulipokwama.

Rejea; Yeye hawaondolei macho yake wenye haki; Lakini pamoja na wafalme huwaweka Katika viti vya enzi milele, nao hutukuzwa. Ayubu 36 :7 SUV.

4. Tunafunguliwa katika vifungo vya mateso.

Watu wengi wamefungwa katika dhambi, wamekuwa wakiteswa na kutumikishwa na shetani bila wao kujijua. Mtu anakuwa mtumwa wa dhambi kiasi kwamba hata ukimwambia hicho unachofanya hakimpendezi Mungu. Anaona unambania au unamfuatilia sana mambo yake.

Wengine hujivuna matendo yao maovu na kujihesabia haki, ndio maana unaweza kukutana na kijana aliyeharibika. Anaweza kumwona kijana mwenzie asiyependa starehe za dunia ni mshamba asiyejua kuendana na kasi ya dunia.

Unapofika wakati wa Mungu, humfungua mtu yule katika vifungo vya mateso, ambayo alikuwa anateswa na shetani. Ndipo unakuta wengine walikuwa wamefungwa katika magonjwa, Mungu anawafungua katika mateso yao na kuwaponya.

Rejea; Nao wakifungwa kwa pingu, Wakitwaliwa kwa kamba za mateso; Ndipo huwaonyesha matendo yao, Na makosa yao, ya kuwa wametenda kwa kujivuna. Ayubu 36 :8-9 SUV.

5. Neno hujachiliwa masikioni mwetu tupate kuacha njia mbaya.

Thamini sana injili inayomhubiri Yesu Kristo, ikiwa tu watu wale watakuwa wanahubiri kweli ya Mungu. Na wakawa wamemtanguliza Mungu katika maombi, uwe na uhakika mtumishi wa Mungu atakaposimama kuhubiri/kufundisha Neno la Mungu, watu watapokea ujumbe ule na fikra zao mbaya litabadilishwa. Maana tayari Mungu atashughulika nao kufungua mioyo yao wapate kusikia Neno lake kupitia mtumishi wake.

Vizuri kumsikiliza Roho Mtakatifu anakutaka useme nini juu ya watu wengine, vizuri kusikiliza Roho Mtakatifu anakuelekeza wapi ukaseme Neno la Mungu. Wakati mwingine unaweza kupata msukumo wa kwenda kuhubiri mahali fulani, ukaangalia mazingira yalivyo ukaogopa kwenda.

Uwe na uhakika Mungu akikuangiza nenda mahali fulani anajua, na atawahudumia kwa jinsi alivyotaka yeye kupitia wewe. Ndio maana unaweza kufundisha somo fulani, watu wakakubali kuokoka, na kuna wakati unaweza kufundisha somo lile lile mahala pengine na watu wasiokoke kwa wakati huo.

Wakati mwingine unaweza kufikiri watu wanakusikia unachokisema juu ya Mungu, kumbe wanakusikia ila hawakuelewi kabisa unachokisema, kwa sababu ufahamu wao unakuwa umefungwa na shetani. Vizuri kujifunza kuwaombea hata wale watakaoenda kusikiliza Neno la Mungu wapate kuelewa ujumbe ulioandaa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Wakati mwingine kama wakristo mnafika hatua mnaanza kwenda kinyume na agizo la Mungu kutokana na mazoea. Lakini Mungu anapotazama hayo hutuma Neno lake mpate kuziacha njia zenu mbaya na kumgeukia yeye.

Rejea; Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu. Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika kufanikiwa, Na miaka yao katika furaha. Ayubu 36 :10-11 SUV.

Wangapi wameambiwa okoka wakakataa, siku za kifo zinawakuta pasipo kuokoka. Wanakufa wakiwa wamekataa wokovu. Ila wapo ambao wanakufa pasipo kuisikia kweli ya Mungu, hao wanapaswa kufikishiwa injili ya Yesu Kristo wasije wakasema hawakusikia.

Rejea; Lakini wasiposikia, wataangamia kwa upanga, Nao watakufa pasipo maarifa. Ayubu 36 :12.

Mungu wetu anatupenda, anapenda tuziache njia zetu mbaya na kumgeukia yeye. Lakini huwa tunakuwa wagumu kuelewa, badala yake tunafia dhambini. Wewe unayesoma ujumbe huu usikubali kufia dhambini, mgeukie Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wako.

Mungu atusaidie tuweze kuithamini hii Neema ya wokovu tuliyoipata bure, ili na wengine wasiomjua Yesu Kristo waweze kumjua kupitia sisi tuliopata neema ya kuokoka. Tukayaacha matendo ya kale na kugeukia matendo mema.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma hapa, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu
Imeandaliwa na Samson Ernest.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.