“Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo”, Kol 3:23‭-‬24 SUV.

Mtume Paulo anawasihi sana Wakristo wahesabu kazi zote kuwa ni huduma inayotolewa kwa Bwana Yesu.

Tunapaswa kufanya kazi kana kwamba Yesu Kristo ndiye Mwajiri wetu, tukijua kazi yeyote ile inayofanyika ni kwa ajili ya Bwana na siku moja tutalipwa kwa kile tulifanya.

Tukiwa na mtazamo huu, tutafanya kazi kwa bidii sana na tutazaa matunda mengi kwa utendaji wetu mzuri wa kazi.

Wakati mwingine huwa tunafanya kazi ya Mungu au maofisini kwa ulegevu mkubwa tukifiri kuwa tunamfanyia mtu fulani.

Mtu akiwa kazini kwa mtazamo huo anaweza kufanya kwa uzembe mkubwa, tofauti na yule anayefanya akijua malipo yake makubwa yapo kwa Mungu.

Tunapaswa kuelewa utendaji wetu wa kazi ya Mungu utatolewa hesabu mbinguni, wapo watu watapokea taji kwa utendaji Bora.

Nafasi yeyote anayokuwepo mtu anapaswa kuitumikia kwa viwango vikubwa na kwa ustadi mzuri akijua anamfanyia Bwana.

Miaka michache iliyopita nimejifunza sana hii, nimefanyia kazi kwa vitendo na niliona matokeo yake mazuri, na kutambua ipo faida kubwa kwa mtu anayefanya kazi kwa bidii na kwa Moyo.

Baada ya kusoma maandiko haya na mengine yanayosisitiza kufanya kazi kwa bidii, nimeona kuna faida za kuonekana kwa macho ya nyama kabisa.

Usifanye kazi ya Mungu kwa ulegevu, ziwe za kutumia mikono au akili, usifanye kazi kwa ulegevu, ofisini kwako ulipoajiriwa usifanye kazi kwa ulegevu, chochote halali usikifanye kwa ulegevu.

Moja ya mtu anayebarikiwa sana na Mungu ni yule anayefanya mambo kwa bidii, kwa Moyo wake wote, kwa akili zake zote, kwa roho yake yote.

Bora kusema hufanyi kuliko kufanya kwa ulegevu, hakikisha unafanya kwa ubora chochote halali kinachopita kwenye mikono yako.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081