Haleluya,
Kuna kuingilia mazungumzo usiyojua yalianzia wapi, unaingia katikati ya mazungumzo na kuanza kuongea yako. Bila kujua jambo limeanzia wapi, wala bila kuuliza watu wameanzia wapi, wewe unadakia mada kwa mbele.
Siku moja tukiwa kwenye mada kali sana inayohusu imani yetu, tulikuwa eneo la uwazi kabisa. Kwa hiyo kila mtu alikuwa na uwezo wa kutusikiliza, mada ilikuwa ya moto sana ikijadili mambo mbalimbali.
Mada hii iliwavutia wapita njia wengi sana, wengine wakawa wanashindwa kupita hivi hivi. Mpaka mwisho wa siku tukapata wageni wawili ambao wote walikuwa wachungaji. Bila kujua mada imeanzia wapi, mchungaji mmoja wapo alidakia ile mada, akaanza kuongea yake, na mwisho wa siku aliongea maneno ambayo hayakuhusiana kabisa na mada iliyokuwa mezani.
Tunasema mkubwa hakosei, ila biblia haisemi hivyo, huyu mchungaji alikosea kwa sababu hakujua mada imetoka wapi na inaelekea wapi. Kwa kifupi aliingilia mazungumzo asiyojua mwanzo wake ni nini, huenda angetulia na kujua mzizi wa mazungumzo yale angejibu vizuri.
Kushusha heshima yako mbele za watu ni rahisi sana, unapaswa kujifunza kusikiliza sana kuliko kuongea. Kuongea iwe nadra sana ila kuwa mtulivu muda mwingi wakati wengine wanaongea. Ili wakati ukifika unatoa maoni yako, yawe ni maoni yaliyoshiba kisawasawa.
Wakati mwingine sio lazima kuongea, nyamaza kimya mpaka pale utakapoombwa utoe neno. Hii inakuondoa kwenye eneo la kuonekana umekurupuka, na kuonekana mtu makini anayejua anachokisema.
Shida yetu huwa hatupendi maarifa sahihi kama haya, muda mwingine tumeongea kiasi kwamba tumevuka mipaka. Hii ni kwa sababu ya kukosa break ya mdomo.
Maandiko yapo wapi katika hili, usiwe mtu wa kudakia mazungumzo kwa mbele. Ukikuta watu wana mazungumzo yao, kama una nafasi ya kujiunga nao, tulia kwanza ujue wanaongelea nini. Usidakie mada kwa mbele bila kuelewa wanazungumzia nini.
Jana nilienda mahali kwa rafiki yangu, bahati nikakuta ana wageni, kawaida yangu nikikuta watu wana mazungumzo yao. Huwa nauliza kwanza mazungumzo haya napaswa kuyasikia au niwaache kwanza mmalize, majibu yao ndio yatanipa ruhusa ya kubaki au kuondoka.
Wakati mwingine huwa siulizi kabisa kutokana na mazingira nitakayoyakuta, naweza kusalimia na kuondoka. Huu ni utaratibu wangu, sasa nilivyoona wale ndugu mazungumzo yao sio ya kumfanya mtu mwingine asisiikie niliungana nao.
Baada ya kuungana na hawa ndugu, alikuja ndugu mwingine, hakujua kilichokuwa kinazungumzwa. Yeye alidakia kwa mbele, binafsi nilisikia moyoni aliwakera watu wale. Maana mpaka alitulizwa kwanza ili mada husika iendelee.
Sio wakati wote tunaweza kuwa sahihi, kuna mahali tunaweza kukosea kutokana na malezi tuliyolelewa. Ama kutokana na kutokuwa na maarifa ya kutosha ndani mwetu.
Usijibu wala usiongee chochote bila kujua unachotaka kuzungumza ni kitu gani, kutofanya hivyo utajiepusha sana na kuonekana mtu anayekurupukia mambo.
Rejea: Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. MIT. 18:13 SUV.
Usikivu ni mhimu sana, usiwe kwenye kusikiliza huku unawaza huyo anayeongea amalize ili uulize swali au uchangie hoja. Hutokuwa na kitu cha kuweka moyoni mwako maana akili yako yote itakuwa inawaza maswali au kukosoa.
Mungu akusaidie uweze kutambua haya ninayokueleza hapa.
Facebook; Chapeo Ya Wokovu
Email; chapeo@chapeotz.com
Blog; www.chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081