
Kila mmoja ana ka historia chake kabla hajaokoka, kanaweza kakawa kahistoria kabaya sana au kanaweza kakawa kahistoria cha kutisha sana.
Hadi mtu kufika hatua anaamua kuokoka, wengine sio kana kwamba waliokoka hivi hivi, wapo walikutana na pigo la nguvu hadi wakaamua kuachana na mambo mabaya ya kumkasirisha Mungu.
Hasa wale watu waliokuwa wabishi sana, watu waliojisemea kabisa hawawezi kuokoka kabisa, watu waliokuwa wakisikia habari ya kuokoka ni kama vile wametukanwa tusi baya sana.
Watu ambao walikuwa hawataki kabisa kusikia habari za Yesu Kristo, wakisikia jina la Yesu Kristo linatajwa ni kama umetaja jina ambalo halifai kabisa.
Wapo wengine wazazi wao waliongea mpaka wakachoka, na wakafika hatua wakasema basi, kama mtoto alikuwa jambazi, wakawa wanasubiri siku wameambiwa njooni mmchukue mtoto wenu mkazike.
Wapo wazazi/ndugu waliongea sana kwa binti yao kuhusu tabia yake mbaya ya ukahaba, baadaye wakaona hasikii na anaendelea kufanya uchafu wake.
Wapo wanawake wameongea sana kuhusu waume zao wenye tabia ya kutembea na wanawake hovyo, wakaomba sana Mungu wakafika mahali wakaona haiwezekani tena kubadilika.
Siku Yesu Kristo anaamua kushughulika na mtu huyo, lazima akubali kufuata kile aliambiwa sana nyuma akagoma, awe anapenda au hapendi, atakubali tu wakati amebanwa na shida ambayo haina msaada mahali popote zaidi ya kwa Yesu Kristo.
Rejea: Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. MDO 22:6-8 SUV.
Hili tunajifunza kwa Sauli ambaye alikuja kuitwa mtume Paulo, alikuwa ni mtu ambaye alihusika na matukio mengi sana mabaya. Aliua sana watu kwa ajili ya jina la Yesu Kristo, lakini ilipofika saa Yesu mwenyewe alisema naye uso kwa uso.
Historia ya Sauli iligeuka ghafla, alijulikana kama muuaji ghafla akageuka mtume wa Yesu Kristo, sawa na mtu ulikuwa unamjua kabisa ana tabia mbaya ghafla ukamwona akawa ni mtu mzuri tena anayemtumikia Mungu.
Historia mbaya ya mtu inaweza ikageuka, haijalishi mtu alikuwa na tabia gani mbaya, Yesu Kristo akiingia ndani ya moyo wake, atakuwa mtu mzuri kabisa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com