Akina mama wana mchango mkubwa sana kwa binti zao, wanaweza kuwafunza tabia njema, pia wanaweza kuwafunza tabia mbaya.

Katika kuwafunza tabia binti zao, zipo tabia binti zao watajifunza kwa kutazama/kuwaona. Na zipo tabia za kufundishwa kwa kuelekezwa namna ya kufanya vitu au namna ya kuishi.

Ukiachana na tabia za kujifunza huko nje, mama ana mchango mkubwa sana kumfunza binti yake tabia njema. Kabla hata ya watu wabaya hawajapata nafasi ya kumpandikiza tabia mbaya, watakuta mama ameshaweka misingi imara.

Ukikutana na binti hajui kupika chakula, ujue mama yake hajamfundisha ama yeye mwenyewe mama hajui kupika. Kama mama anajua kupika ujue amemlea vibaya binti yake, labda kwa sababu ya kuwa na mfanyakazi wa ndani.

Ukiona binti ameolewa, alafu kila siku makelele ndani ya ndoa yake, mwanaume anafika mahali anachoka makelele yake. Rudi nyuma mwangalie mama yake, utakuta hali ni ile ile, yaani alivyo binti yake ndivyo alivyo mama yake.

Ukiona binti mchafu, hapendi kufua nguo zake, hapendi kuoga au kusafisha mwili wake, hapendi kusafisha nyumba, hapendi kufua mashuka yake ya kulalia. Ndivyo alivyo na mama yake vivyo hivyo.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili suala, huenda ukaanza kusema kila kitu sisi wamama na kwanini wasiwe wababa?

Rejea: Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.EZE. 16:44 SUV.

Kuwa mama bora, unamtengeneza na binti yako kuja kuwa mama bora. Hakikisha unasimama katika zamu yako kama mama, hata kama una mtu anayekusaidia kazi zako ila hakikisha unakuwa makini kwa binti yako.

Malezi yako yana mchango mkubwa sana kwa binti yako, vile ulivyo na unavyoishi ni mchango mkubwa sana kwa binti yako. Kuna vitu anavyokopi kama vilivyo kutoka kwako, kama una tabia ya kumkemea mume wako mbele ya binti yako. Uwe na uhakika akiolewa naye ataenda kuwa vivyo hivyo.

Kama mume wako anaandaliwaga chakula chake na dada wa kazi, uwe na uhakika na binti yako atakuwa vivyo hivyo kwa mume wake. Anaweza kukutana na somo la kumwandalia mume wake chakula, akalipuuza hilo somo kwa sababu ya mama yake alikuwa anamwachia hiyo kazi dada wa kazi.

Nimalize kwa kusema, hakuna tabia isiyoweza kurekebishika, kama mama ulikuwa na tabia za mama yako, na tabia hizo unaona sio nzuri. Hakikisha unaziacha ili kumsaidia binti yako, usipofanya hivyo utakuwa unaendeleza kizazi kibovu.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.