Huruma ipo kwa mwanadamu, hata kama utakutana na jambazi anayeua watu bila hofu yeyote kama vile anachinja mbuzi. Kuna mahali anaweza kufika akajawa na huruma, akashindwa kutelekeza wajibu wake wa kuua.
Mungu ametuumbia hiyo hali ndani yetu, Mungu anajua ilipaswa kuwepo ndani yetu, na Mungu anaitumia kwetu kutekeleza jambo fulani analotutaka tuwajibike nalo.
Huruma hii inaweza kutumika vizuri kwa watu baadhi, na wengine wasiojua vizuri matumizi yake sahihi. Huwa wanaitumia vibaya na kupelekea kumkosea Mungu wao, wakisema hawana namna ya kufanya.
Kama ulikuwa hujui ni kwamba, kuna vitu hupaswi kuviruhumia kabisa katika maisha yako. Hupaswi kumhurumia rafiki ambaye anakufanya kila siku umkosee Mungu wako.
Hupaswi kumhurumia kaka/baba anayekutaka kimapenzi, alafu wewe bado ni binti ambaye hujaolewa au umeolewa ila sio mume wako. Huyo hupaswi kucheka naye hata sekunde moja, ikiwa kweli unampenda Mungu wako.
Hupaswi kuwaonea huruma marafiki wanaokupandikiza roho mbaya ndani yako, hawa unapaswa kuachana nao kabisa. Hakuna kujadili mara mbili mbili labda ufanyaje, kaa nao mbali.
Hupaswi kuwa na rafiki ambaye anakushauri kubomoa nyumba yako, huyu usimhurumie kabisa, kaa naye mbali tena umbali wa kutosha haswa.
Usikubali kung’ang’ana na jambo linalokufanya umkosee Mungu wako kila siku, hata kama kuna faida za nje unapata. Bila kuweka huruma zako, achana nalo kabisa.
Unapoachana nalo hilo linalokukosesha na Mungu wako, huko ndio tunaita kukata matawi yasiyofaa. Hata kama tawi la mti linaonekana ni nzuri sana, kama halifai utapaswa kuliondoa.
Sasa wengi tunashindwa kuondoa matawi mabovu, tunakuwa na huruma nyingi kiasi kwamba tunakuwa tunamtukuza shetani bila kujua. Badala ya kumtukuza Mungu, tunakuwa tunamtukuza shetani kwa kung’ang’ana na mambo yasiyofaa.
Mungu wetu hana huruma na mambo mabaya, anapochukizwa na jambo baya, hawezi kufurahishwa na uchafu wa mwanadamu eti kwa sababu alimuumba kwa mfano wa sura yake.
Mungu hafurahishwi na mabaya yako, wala hakuna ofa ya kuingia mbinguni kwa watenda mabaya/dhambi. Hilo Mungu hawezi kuwa na huruma nalo kwako, kama huwezi kubadilika na ukaachana na maovu yako, jehanamu inakusubiria.
Rejea: Kwa sababu hiyo, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa kuwa umepatia unajisi patakatifu pangu, kwa matendo yako yote niyachukiayo, na kwa machukizo yako yote, kwa sababu hiyo mimi nami nitakupunguza; wala jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma. EZE. 5:11 SUV.
Ukiwa kama mtoto wa Mungu, uliyezaliwa mara ya pili, kwa maji na kwa Roho Mtakatifu, huwezi kuwa na huruma na uchafu wa aina yeyote ile. Maana unajua madhara yake kwenye maisha yako ya kiroho.
Ukiona mtu anafanya dhambi kwa ujasiri na ukijaribu kumtoa katika mazingira ya dhambi, anajaribu kukupa sababu nyingi za kuonea huruma hicho unachomsihi akiache. Uwe na uhakika Roho Mtakatifu ameshaondoka siku nyingi ndani yake, yeyote mwenye Roho wa Mungu ndani yake, hawezi kuonea huruma chochote kinachomfakaranisha na Mungu wake.
Sijui wewe unaonea nini huruma katika maisha yako, ikiwa Mungu hawezi kuja kukuonea huruma siku ya mwisho. Unapaswa kujitafakari kwa upya na kwa kina zaidi.
Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.