
Kama kuna jambo la kujivunia katika maisha yetu ni kuwa na Yesu Kristo, na la pili kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Yesu Kristo akiwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, na ukawa unaishi maisha matakatifu, haijalishi upo maeneo ambayo yanakufanya usiwe huru sana kumtumikia Mungu wako.
Ikiwa utaweza kutunza ushuhuda wako katikati ya mahali ambapo ulikuwa unakandamizwa, Mungu atakuheshemu sana.
Tunapoendelea kujifunza habari za Yusuf, hapa tunaona vile Mungu aliachilia kibali kwake kiasi kwamba Farao alikuwa anampa ruhusa ya kufanya vitu ambavyo kwa hali ya kawaida ingekuwa ngumu sana.
Rejea: nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu. MWA. 47:6 SUV.
Unaona hapo, Farao alimpa uhuru mkubwa sana, huru ambao pasipo Mungu asingeweza kuwa nao. Ndugu zake wote alikuwa na uwezo kuwapa nafasi za kazi kutokana na ruhusa aliyopewa na Farao.
Hata leo inawezekana kabisa ukapata kibali kwa wakuu, vile unavyomheshimu Mungu wako utakuwa unaona unapata kibali maeneo mengi.
Hata kama kwa sasa unapitia wakati wa kudharauliwa sana, uwe na uhakika ipo siku inakuja utaona ukipata kibali.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com