Kiburi kimekuwa ni kaburi la wengi kuzikwa hatua zao kubwa walizofika kihuduma, wengi sana huduma zao zilikufa baada ya kuinuka kwa kiburi chao.

Hasa mtu anapofika kiwango fulani cha utumishi alionao, wengi sana hushindwa kujizuia na kuanza kujaa kiburi kingi.

Hii inatokea kwa sababu wengi wetu huwa hatupendi kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu, mtu yeyote anayelijua Neno la Mungu vizuri. Hawezi kuwa na kiburi chochote, zaidi atakuwa mnyenyekevu zaidi.

Wengi wetu huwa tunafikiri kuwa mwombaji mzuri inatosha kuwa mkristo mkamilifu, badala yake wengi tumesahau Neno la Mungu. Ambalo linatusaidia maeneo mengi sana katika maisha yetu.

Neno la Mungu linampa mtu hekima za kutosha, na kujifunza kwa watumishi wengine walioanza huduma siku nyingi napo kuna vitu vizuri vya kujifunza kwao.

Kitu kingine ambacho kimewafanya watu wawe na kiburi ni kutokubali kuwa chini ya baba wa kiroho, wengi sana wanaonguka kwenye mtego wa kiburi ni wale wasiokubali kuwa chini ya baba wa kiroho.

Kiburi ni sumu mbaya sana kwa mkristo yeyote yule, kiburi ni sumu mbaya sana kwa mtumishi yeyote wa Mungu. Haijalishi una huduma gani ya viwango vya juu, ukishaona kiburi kimeinuka ndani yako, vyema ukajiwahi haraka mbele za Mungu.

Kiburi hakijawahi kumwacha mtu salama, tena kiburi kinakusababisha ushushwe na Mungu haraka sana kwenye nafasi uliyokuwa nayo.

Rejea: Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. OBA. 1:3‭-‬4 SUV.

Kadri Mungu anavyozidi kukuinua kwenye maisha yako, inaweza ikawa kwenye biashara zako, kazi yako, na huduma yako. Unapaswa kuendelea kuwa mnyenyekevu zaidi mbele za Mungu, ndio maana ni muhimu sana kutokaukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako.

Kiburi asili yake kinatoka kwa shetani, Shetani anaweza kutumia nafasi yako uliyofikia kukufanya ufarakane na Mungu wako haraka sana.

Lisha ya kiburi ni dhambi mbele za Mungu, kiburi chako kinaweza kugeuka kero kubwa sana mbele za watu. Hujawahi kuona mtu mwenye kiburi anavyosumbua sana? Bila shaka umewahi kukutana na mtu wa namna hiyo.

Kataa kabisa roho ya kiburi ndani yako, kiburi kitakufanya ushushwe haraka sana kwenye viwango ulivyofikia, tena utashushwa na Mungu mwenyewe. Epuka sana hili, usije ukakutwa na hili janga la kujitakia mwenyewe.

Mungu akubariki sana.
Imeandikwa na Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.