Vipo vitu hupaswi kujiamini mpaka ukapitiliza, hasa vile vitu vyenye nia mbaya na wewe, bora kuonekana muoga kuliko kutulia mahali ambapo unaona usalama wa maisha yako upo hatarini.

Kukimbia kunaepusha mengi, unaweza kuokoa uhai wa maisha yako kwa kukimbia, unaweza kusema hutishwi na chochote, ukasubiri wenye nia mbaya wakafanya kile wanachotaka kufanya kwako. Ukapoteza uhai wako kwa kujiamini kupita kiasi.

Mungu ametupa akili nyingi sana, unaweza ukawa umeokoka vizuri kabisa, ila usipotumia vizuri akili alizotupa Mungu. Kuna mambo mengi sana yanaweza kutuangamiza, kwa sababu ya kupuuza na kuyaona hayo mambo hayawezi kukufanya chochote.

Kuna mahali utafika, haitajilisha umeokoka vizuri sana, utapaswa kukimbia ili kuokoa uhai wako, watu wanaweza kukuona kuwa ni mtu muoga sana. Hilo lisikupe tabu, maana unajua unachofanya ni kwa ajili ya usalama wa maisha yako.

Acha kuwa mjinga, unaona watu wanakujia na mapanga, badala ya kukimbia, unatulia tu, nakwambia utakufa kizembe. Kwanini ufe kizembe au kwanini upate majeraha kwenye mwili wako, na wakati ulikuwa na uwezo wa kukimbia.

Dada unaona kabisa kuna mazingira fulani yanatengezwa kwa ajili ya kubakwa, unaendelea kutulia tu mazingira yale kwa sababu unajiona umeokoka. Acha uzembe, unapaswa kukimbia haraka sana, ukizumbaa utafanyiwa kitu kibaya na kubaki kumlaumu shetani.

Kuokoka kwetu sio kana kwamba kunatufanya tuache kutumia akili zetu, tena mtu yeyote aliyempokea Yesu Kristo anapaswa kuwa na akili nyingi zaidi ya asiyeokoka. Badala yake huwa kinyume, wale wasiomjua Kristo wanakuwa na akili kupita waliokoka.

Kuokoka hakukufanyi uwe mjinga, bali kunakufanya uwe na akili zaidi, na kunakufanya uwe mjanja zaidi, usiyeweza kuingizwa kwenye mitengo mibaya kwako.

Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo, kama nasi tumempokea kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu, tunapaswa kujifunza kwake. Tukijifunza kwake au kupitia Neno lake, tutakuwa watu makini na wanaoweza kujiepusha na mazingira hatarishi kwetu.

Rejea: Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni. YN. 8:59 SUV.

Yesu Kristo alivyoona wayahudi wanataka kumpiga mawe, Yesu Kristo alijificha na kuondoka hekaluni. Kama Yesu Kristo alikimbia, wewe ni nani ambaye hutaki kujiepusha na watu wenye nia mbaya na wewe.

Wewe ni nani usiyetaka kujihami na hatari unayoona inaenda kukuangamiza maisha yako, usikubali kitu kama hicho, hakikisha unakimbia. Hapo utakuwa umejiepusha na mtego uliokuwa umeandaliwa kwa ajili yako.

Kama ni mtumishi wa Mungu, unaona kuna mtego wa ngono kwa mshirika uliyeenda kwake kumfanyia huduma ya maombi. Tumia akili yako yote kujiepusha na hayo mazingira yenye nia mbaya na wewe, fanya ufanyavyo usinase kwenye mtego huo.

Upo mahali unafanya huduma, ukaona kuna mazingira fulani sio salama kwako, jiepusha na hayo mazingira, utakuwa hujafanya kosa lolote.

Hiyo ndio akili ya watu wenye Kristo ndani yao, usikubali kufa kizembe, Yesu Kristo anatusaidia sawa, ila nasi pia tunapaswa kutumia uwezo wa akili aliotupa ndani yetu. Usiingie kwa makusudi kwenye mtego uliotegwa kwa ajili yako, epuka mtego huo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com