Kila mmoja wetu anapenda kuhakikishiwa usalama wa maisha yake, hasa anapokuwa na mashaka na kitu fulani, yule anayekifahamu hicho kinachompa mashaka anapaswa kumhakikishia usalama wa hicho kitu.

Unaweza kwenda duka la simu kununua simu, kitakachokusukuma zaidi ununue simu sio tu uzuri wa kava la simu, bali ni kuhakikishiwa uimara wa simu hiyo. Ukishapewa sifa za simu unayotaka kununua, inakuwa rahisi kwako kuinunua hiyo simu.

Ila unapokutana na muuzaji ambaye anakuwa na wasiwasi kwa kile anauza, hata ule uhitaji wa simu uliokuwa nao, utaisha ghafla kutokana na muuzaji mwenyewe kuwa na mashaka kwa kile anauza.

Wadada wengi wanaojitambua, kabla ya kukimbilia kuolewa na mwanaume fulani, huwa wanataka kuhakikishiwa usalama wa maisha yao. Sio kuhakikishiwa kwa kuambiwa, huwa wanataka kujithibitishia wenyewe kwa kumsikiliza mhusika au Mungu anasemaje kuhusu huyo aliyewajia.

Wanapoona yule mwanaume anayetaka kuwaoa, anakuwa na mashaka mashaka, huwa wanaanza kupata wasiwasi juu ya yule mwanaume. Shida haswa ni nini? Mwanaume yule ameshindwa kuwahakikishia usalama wao.

Utasema bado hawajamjua Mungu vizuri, Kabla hujasema hivyo nikuombe urudi kwako binafsi, unapoenda dukani kununua kitu. Hata kama hicho kitu huwa unakinunua kila siku, ikatokea muuzaji akawa na wasiwasi na kile anauza.

Bila kuambiwa na mtu, utaanza kupata hofu juu ya hicho unachotaka kununua, kilichokufanya uanze kupata maswali mengi yanayokupelekea upate wasiwasi au hofu ni kutokana na muuzaji mwenyewe.

Ndivyo ilivyo wadada wanaothamini utu wao, hawezi kujitupia hovyo kwa mwanaume kwa sababu ana uhitaji wa kuolewa, kama mwanaume huyo hatamthibitishia vizuri usalama wa maisha yake ndani ya ndoa yake. Huyo mwanaume anaweza asikubalike.

Inawezekana hapo ulipo umechoka sana, huoni tumaini la maisha yako tena, hii ni kutokana na kukosa uhakika wa jambo fulani. Inaweza ikawa ni ajira, inaweza ikawa ni mume, inaweza ikawa ni mke, inaweza ikawa ni mtoto, inaweza ikawa ni shule, inaweza ikawa ni kupona ugonjwa unaokusumbua, na mengine mengi ya kufanana na hayo.

Umekosa uhakika ndio maana umejikunyata kama mkiwa, katika hali ile ile ya kuchoka, akatokea mtu akakupa uhakika wa kile ambacho ulikuwa umekosa tumaini. Utaweza kupata nguvu mpya na ujasiri mkubwa, hali ambayo inaweza kuleta mshangao kwa ndugu zako au marafiki zako.

Hili tunajifunza kwa watu hawa waliokosa tumaini katika maisha yao, lakini mtume Paulo alipowahakikishia usalama wa maisha yao. Walipata nguvu ghafla, wakachangamka na kula chakula wenyewe.

Rejea: Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea. Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula. Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe. MDO 27:34‭-‬36 SUV.

Ndugu unahitaji uhakikisho, umechoka na huoni haja ya kuishi tena katika Dunia hii iliyokosa huruma kwako, kwa sababu ya kukosa uhakika wa maisha yako.

Huenda hapo ulipo hujala chakula na una njaa ila huna hamu ya kula kabisa, tatizo sio hiyo shida iliyokupata, tatizo ni kukosa uhakika wa maisha yako, ukipata uhakika wa maisha yako utashangaa moyo wako ukichangamka tena kwa upya.

Kupitia andiko hili takatifu, nakuambia kwamba mwenye haki hajawahi kuachwa na Mungu, usife moyo bado asubuhi sana, jioni bado, nikiwa na maana Mungu anajua shida yako.

Pamoja na watu walikuambia usifanye hilo, wewe ukafanya na unaona shida uliyokutana nayo baada ya kukataa kusikiliza ushauri uliopewa. Bado unayo nafasi ya kutubu mbele za Mungu na Mungu akaanza kutembea na wewe kwa upya.

Ulikosea sawa, huna haja ya kujiona hufai tena, unafaa sana mbele za Mungu, cha msingi ni kumrudia Mungu kwa toba, utaona badiliko ndani ya moyo wako.

Usijikatie tamaa kwa sababu yeyote ile, mambo yako hayajaenda vile ulitaka yaende, bado Mungu hajasema hutopata tena, ipo nafasi nyingine zaidi. Ukiwa mvumilivu na ukajua siku yako ipo, hutoyumbishwa tena kwenye maisha yako ya wokovu.

Uhakika tayari umeshakuwa nao maana umemwamini Yesu Kristo, huu ndio uthibitisho wako, huna haja ya kutafuta mtu mwingine akusaidie, unao uthibitisho ndani yako. Umebeba jina kuu ndani ya moyo wako, jina la Yesu Kristo, huna haja ya kukosa uhakika wa maisha yako.

Muhimu; kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi uchukue hatua ya kujiunga na kundi hili. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com