Tunaweza kuwachukia wengine vile wanavyotukemea, au vile wanavyokasirika mbele yetu, tunaona ni wabaya wetu au tunaanza kuwatazama kwa jicho la kutowafurahia.

Tunaweza kumwona mzazi ni mbaya kutokana na anavyokukemea kwa nguvu kwa kufanya kosa fulani au kutokufanya jambo alilokuambia ulifanye. Wakati mwingine inafika mahali unamwona mzazi wako hakupendi, na ana chuki na achuki na wewe.

Wengine ni ndani ya ndoa zao, wanapoona waume/wake zao wanakasirika au wanakuwa wakali kwenye maeneo fulani, wanaanza kuona huenda upendo haupo kwa waume/wake zao. Bila kukaa chini na kujiuliza maswali wapi wanakwama na kusababisha hayo yote.

Wapo watu maofisini wanachukia viongozi wao vile wanavyokasirika mbele yao na kuwaonya juu ya tabia fulani mbaya, na kuwaelekeza wanayopaswa kufanya katika nafasi zao za ajira.

Kuna watu mahusiano yao ya uchumba yamevunjika kutokana na mmoja wao kushindwa kuzingatia vitu vidogo vidogo anavyoambiwa na mwenzake, ambavyo vina umhimu mkubwa sana katika kuleta uhai wa mahusiano yao ya uchumba.

Hayo yote niliyoyasema na mengine ambayo sijayasema na yanaendana na hayo niliyotangulia kusema, huwa yanasababishwa na moja ya jambo hili ambalo ninaenda kukueleza hapa.

Hili jambo sio tu kwenye maeneo hayo niliyotangulia kusema, hili linaingia hadi kwenye eneo la kiroho, yapo mambo huwa tunamkosea sana Mungu wetu kwa sababu hii hapa;

Kinachoturudisha nyuma au kinachotukwamisha au kinachotufelisha mitihani mingi katika maisha yetu, au kinachotufanya tusifanikiwe baadhi ya mambo ni “kutozingatia maelekezo au ni kupuuza maelekezo muhimu tunayopewa.”

Mtu anaweza kuambiwa ufanye hivi na vile, na usifanye chochote nje na maelekezo muhimu uliyopewa, mtu huyo anafika mahali anaenda kufanya kile kile alichozuiliwa au alichokatazwa asifanye.

Hili tunajifunza kwa wana wa Israel, vile ambavyo walipaswa kufanya wakati Bwana atapowashushia chakula kutoka mbinguni. Kila mmoja alifikiwa na maelekezo muhimu watakayofanya wakati huo.

Rejea: Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. KUT. 16:16 SUV.

Baada ya hapo, wapo ambao walifanya vile ambavyo walipaswa kufanya, na wapo wengine ambao walifanya visivyotakiwa kufanyika. Wale ambao walifanya vile ambavyo walipaswa kufanya hawakupungukiwa, na wale ambao walifanya visivyotakiwa kufanyika walipungukiwa.

Rejea: Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa. KUT. 16:17‭-‬18 SUV.

Tatizo lipo wapi hapa? Tatizo lipo kwenye eneo la kutosikiliza maelekezo muhimu anayopewa mtu, sio kana kwamba mtu anakuwa hasikii anachoambiwa. Kusikiliza anakuwa anasikiliza vizuri sana ila wakati wa kutekeleza au kutenda, inakuwa tofauti kabisa na maelekezo aliyopewa.

Hawa wana wa Israel hamsikiliza Musa, wakati maelekezo aliyopewa awaambie yalikuwa yanatoka kwa Mungu mwenyewe. Wao wakaamua kufanya vile ambavyo wanajua wao.

Rejea: Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. KUT. 16:20 SUV.

Ona matokeo mabaya ya kutosikiliza maelekezo waliyopewa, chakula walichobeba kilikuwa nje na matumizi yao, tena nje na maelekezo waliyopewa na Mungu mwenyewe kupitia kinywa cha Musa.

Kutosikiliza kwao maelekezo waliyopewa, matokeo mabaya yalimfanya Musa awakasirikie sana kama tunavyosoma hapo kwenye mstari niliyokupa hapo. Ambapo hili jambo linawakumbuka watumishi wengi sana wa Mungu, hasa wale ambao wanachunga kanisa/makanisa.

Wapo watu wanapoona wamekasirikiwa badala ya kuomba msamaha huwa wanafikiri wameonewa, na wengine huwa wanafikiri hawapendwi. Watu kama hawa huwa ni vigumu sana kuwasaidia.

Changamoto kama hii sio tu Musa amekutana nayo, wapo wachungaji wengi wa makanisa wanakutana nayo leo, wapo waume/wake wanakutana nayo, wapo viongozi wa serikali wanakutana nayo.

Kama unataka kufanikiwa katika maisha yako ya kiroho au kimwili, yaani kwenye biashara yako, ndoa yako, masomo yako, huduma yako, uongozi wako, unapaswa kuzingatia maelekezo muhimu unayopewa.

Sisi wakristo maelekezo muhimu tunapewa kupitia usomaji wa Neno la Mungu, au vitabu mbalimbali vya watumishi wa Mungu, au kupitia mafundisho mbalimbali kwa njia TV, CD, DVD na nk.

Mungu akusaidie sana katika hili, ili uweze kufanikiwa katika maisha yako, ndipo utaona ndoa yako ikidumu, kazi yako ikienda vizuri, masomo yako yakienda vizuri, biashara yako ikienda vizuri, huduma yako ikienda vizuri, na mengine mengi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081