Atukuzwe YESU Kristo aliye hai, kwa ulinzi na uzima wake. Saa nyingine tena ya kwenda kushirikishana tafakari nzuri ya Neno la Mungu.
Kila mmoja aliye ndani ya kanisa amejaliwa kitu cha kufanya, si kwa mashindano wala si kwa majivuno. Lipo jambo kwa mtumishi wake, Mungu anamtaka alitende ndani ya hema yake.
Wapo waimbaji ambao wakisimama kumwimbia Bwana, watu wanaponywa magonjwa yao, waliokata tamaa wanainuliwa tena, waliovunjwa mioyo yao wanapata tumaini jipya la kusonga mbele.
Wapo wahasibu wanaweza kupokea fedha na kutunza hazina hiyo hekaluni mwa Bwana, kusimama kwao katika zamu zao. Kunalifanya kanisa liweze kuendeshwa vizuri kupitia mahitaji mbalimbali yanayohitaji fedha kutumika.
Wapo wapambaji wanaweza kusimamia kanisa na kulipamba kanisa likakaa vizuri, kila atakayeingia hemani mwa Bwana anabarikiwa tu na mwenekano wa hema la kumwabudia Mungu. Kupamba kwao kunaweza kusionekane sana mbele za watu wengine, ila mbele za Mungu ni baraka kubwa mno.
Wapo walinzi wanaweza kusimama kwenye malango ya hema la kuabudia, kwa ajili wa kuangalia hali ya usalama wa kanisa na mali zake. Hawa wanaweza kuonekana ni watu wenye hali za chini sana, ila wana umhimu mkubwa sana kwa kanisa.
Wapo watu kazi yao ni kufanya usafi wa kanisa, unaweza kuona kama vile wamekosa kitu cha kufanya. Lakini wanambariki Mungu wao kwa usafi wa hema la kuabudia.
Wapo watumishi ambao Mungu amewateua kwa ajili ya kuhudumia watoto wadogo, ukimkuta na watoto utafurahi mwenyewe. Maana ndani yao Mungu ameweka wito huo ambao hapana mtumishi mwingine anaweza.
Wapo watu wamejaliwa huduma ya ualimu ndani yao, japo hawana nafasi kubwa sana ndani ya kanisa. Ila ukiwakuta wanafundisha Neno la Mungu, utajiuliza mara mbili mbili, kwanini hawana nafasi ndani ya kanisa kuhudumia watu wengine.
Zipo nafasi nyingi sana, wapo watu wanaweza kuinuliwa na Mungu kwa ajili ya kuombea kazi ya Mungu ndani ya kanisa. Japo kwa kawaida wanaweza kuonekana watu wa kawaida, ila wana umhimu mkubwa sana.
Huduma hizi zote zinapaswa kutambuliwa ndani ya kanisa, bila kutambuliwa na kuwekwa vizuri, zinaweza kudidimizwa chini mpaka pale mhusika atakapotambua mahali pa kumtumikia Mungu wake.
Huwezi kulazimisha kufanya kile Mungu anakusukuma ndani yako, ila unapaswa kumwomba Mungu akupe kibali mbele za watu upate kutumikia kusudi lako.
Unaweza kuhangaika kuhama makanisa mbalimbali, ukashangaa kila unapoenda unakutana na hali ileile. Ila kama Mungu amekuongoza sehemu ya kusali, uwe na uhakika atakupa kibali mbele zake.
Sikatai kuwa zipo sehemu ambazo zinaweza kukuzuia kulitumikia kusudi la Mungu, kwa hila tu za shetani. Ila fahamu kuzuiwa kwako ni kwa muda tu, ila upo wakati wa kuinuliwa kwako.
Haya tunajifunza zaidi tunaposoma andiko hili takatifu;
Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa matuo ya BWANA. 2 NYA. 31:2 SUV.
Hapo tunamwona mtumishi wa Mungu Hezekia akaweka mgawanyo wa majukumu kwa kila nafasi ya kuhani na walawi kwa zamu zao.
Kila mmoja alisimama kwa nafasi yake kumtumikia Mungu wake, hakuna aliyemtegea mwenzake. Maana walijua wajibu wao mbele za Mungu.
Je wewe umesimama kwenye nafasi yako? haijalishi unaonekana au hauonekani, simama kwa kile Mungu amekiweka ndani yako kama kuhani. Maana kila aliyempokea Yesu Kristo anayo mamlaka ya kikuhani mbele za Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com