Vipo vitu vinaweza kuwa vyanzo vikubwa vya sisi kushindwa kuendelea mbele, tunaweza tukawa na malengo mazuri kweli ya kufanya vitu vizuri katika maisha yetu. Ila tukawa na kikwazo mbele yetu kinachotukwamisha tushindwe kutimiza/kufikia malengo yetu.

Vipo vikwazo ambavyo vipo ndani ya uwezo wetu, ambavyo tunaweza kuvikataa na maisha yetu yakaendelea vizuri kabisa. Badala ya kuviondoa hivyo vikwazo, wengi wetu tunakuwa tunavikumbatia.

Katika safari yako ya mafanikio unakutana na mtu anayekuvuta nyuma kila hatua unayopiga mbele, kila ukijaribu kusonga mbele unajikuta upo pale pale. Kila ukijaribu kufanya hichi na kile, unashangaa unavutwa nyuma, usimwache huyo mtu.

Unaweza ukakidharau hicho kinachokufanya ushindwe kwenda mbele, kadri unavyokipuuza ndivyo hali unavyozidi kuwa ngumu zaidi. Kadri unavyozidi kusema ngoja kwanza, ndivyo mambo yako yanavyozidi kuwa mabaya zaidi.

Kuna malengo makubwa umejiwekea ila kuna kitu unakiona hakipo sawa, hicho kitu unakiona kabisa usipokiepuka haraka hutoweza kufikia malengo yako uliyojiwekea. Kisa unaogopa lawama kwa watu/marafiki/ndugu zako watakuona una roho mbaya.

Unapaswa kuelewa vipo vitu hupaswi kuvifumbia macho, ukivifumbia macho vinaweza kuua ndoto zako zote ulizokuwa nazo. Ni kama haiwezekani ila unapaswa kuelewa hili, ili uweze kuchukua hatua mapema.

Hili tunajifunza kwenye kisa cha Yona aliyekataa wito wa Mungu kwenda Ninawi, akaona akimbilie Tarshishi.

Rejea: Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA. YON. 1:2‭-‬3 SUV.

Mungu bado alikuwa na Yona, merikebu aliyopanda Yona kukimbilia Tarshishi, merikebu hiyo ilianza kupata shida njiani. Bahari ilichafuka isivyo kawaida, yote hayo yalisababishwa na Yona, yaani kwa lugha ya sasa tunasema chanzo cha matatizo yote kilikuwa ni Yona.

Kupona watu wale ilikuwa lazima wamtoe Yona kwenye Merikebu, uamzi ulikuwa wao, wamwache Yona ndani au wamshushe. Na walivyojaribu kurudi nyuma ilishindikana kabisa, mpaka pale walipomtupa baharini, na bahari ikatulia.

Rejea: Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. YON. 1:15 SUV.

Tunajifunza nini hapa, yapo mambo katika maisha yetu pasipo kuyaondoa, pasipo kuyatupa nje. Maisha yetu ya kiroho hayawezi kuwa salama, lazima tufe kiroho, maana kuna vitu hatukutaka kuviondoa mapema.

Sijui Yona wako ni yupi katika safari yako, ila unapaswa kuhakikisha hulei kitu kinachokufanya uendelee kuwa mbali na Mungu wako.

Hupaswi kuendelea kumkumbatia rafiki anayekuvuta nyuma, vizuri kuachana naye kabisa. Ukileta huruma kama walivyotaka kufanya kwa Yona, merikebu yao isingefika popote.

Rejea: Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda. YON. 1:14 SUV.

Kuna mtu anakuletea kikwazo mbele yako, epukana naye, kaa naye mbali, ili uweze kufika mahali unaenda. Ukiwa na huruma sana uwe na uhakika hutofika popote.

Usikumbatie jambo lolote lisiloendana na maono/malengo yako, litakusumbua sana na usipokuwa mwangalifu safari yako itakuwa imeishia hapo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081