Wasichokijua watu ni kuwa hawawezi kuua ukristo, haijalishi watafanya nini, hawawezi kuua ukristo, kitu watachofanikiwa kukifanya ni kuchoma makanisa  moto ila sio kuua ukristo.

Dhehebu linaweza kusambaratika na kusahaulika kabisa kama lilikuwepo, ila sio ukristo. Kulizimisha jina la Yesu Kristo ni ngumu na haiwezekani kuzimwa, watu wanaomwamini na wanaomcha katika roho na kweli, wataendelea kuwepo.

Unapoona mtu anahaingaika na ukristo hupaswi kuumiza naye kichwa sana, maana hakuna anachoweza kukifanya ukristo ukatoweka au ukafutika kabisa. Tena kadri wanavyozidi kuusonga ndio unazidi kuwa imara zaidi kwa watu wanaoliamini jina la Yesu Kristo.

Haijalishi watawaua sana watumishi wa Mungu wanaolihubiri jina la Yesu Kristo, wale wale Mungu aliowakoa wataendelea kutangaza habari za Yesu Kristo. Mungu atainua mtu ambaye hata hakudhaniwa kama anaweza akawa na uwezo wa kulihubiri Neno la Mungu kwa ujasiri kiasi kile.

Ukristo unaishi, hata kama una nguvu kubwa sana ya kutisha, utafanya kila unaloweza ila nakuhakikishia huwezi kuua ukristo. Mitume wengi sana wa kwanza waliteswa na kuuwawa kikatili, ili waache kutangaza habari njema za Yesu Kristo.

Pamoja na juhudi zote hizo za kutaka kuuzimisha ukristo au kuzimisha habari za Yesu Kristo, hizo juhudi hazikuzaa matunda na badala yake Neno la Mungu liliendelea kusambaa kwa kasi hadi leo mimi na wewe tumepata neema ya kuujua wokovu.

Shetani na watu wake wanazidi kufanya juhudi kubwa sana kuua ukristo, hilo halitakaa liwezekana kamwe, watu wataua miili ila roho zetu zitakuwa salama. Huna haja ya kuwa na hofu yeyote labda ukristo utakufa.

Mafundisho ya neno la Mungu yanaweza yakawa magumu kupatikana ila sio kana kwamba wanaomwamini Yesu Kristo watakosekana, wapo wengi sana, hata kama wanapigwa marufuku.

Hili limeshindikana tangu zamani, Yesu Kristo ataendelea kuhubiriwa kila kona ya Dunia, na watu wengi wataamini na kuokoka. Haijalishi mahali walipo hakuruhusiwi kujengwa kanisa, injili itafika tu.

Tena siku hizi teknolojia ya mawasiliano imerahishisha kila kitu, mitandao ya kijamii imejaa habari za Yesu Kristo. Habari njema zinahubiriwa, usifikiri Neno la Mungu linaanguka bure, wapo watu wanaokoka kupitia mitandao ya kijamii.

Nakueleza kitu ambacho nakutakana nacho kwenye huduma hii ya kumhubiri Yesu Kristo kwenye mitandao ya kijamii, tena wengine walishashindikana kabisa. Lakini Yesu Kristo aliwaokoa, na kuwabadilisha tabia zao mbaya na kuwa watu wazuri.

Napata ujasiri wa kukueleza haya kutokana na Neno la Mungu, tunamwona mtu mmoja aitwaye Sauli, alilaharibu sana kanisa. Aliona hilo halitoshi na kuingia nyumba kwa nyumba na kuwatupa gerezani wanawake kwa wanaume.

Wale waliopata nafasi ya kutawanyika wakaenda huko na kule, waliendelea kuhubiri Neno la Mungu. Kwahiyo Sauli hakuna alichokimaliza, wale waliofungwa gerezani, wapo waliokuwa nje wakaendelea kuhubiri Neno la Mungu.

Rejea: Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.  Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. MDO 8:3‭-‬4 SUV.

Mwanzilishi wa imani hii aliuawa na kufufuka siku ya tatu, kifo na mauti aliishinda, imani yetu ipo hai. Hakuna chochote kitakachoweza kuua imani yetu ya kikristo tena, wokovu tulionao ulipatikana kwa gharama kubwa sana.

Huna haja ya kuogopa chochote, nilikuambia mwanzo dhehebu fulani linaweza likasambaratika kabisa ila sio ukristo. Ukristo upo ndani mioyo ya watu, huwezi kuua, ukiua huyu anainuka yule, vivyo hivyo unaendelea kuwepo hadi Yesu Kristo anarudi kuwachukua watu wake.

Endelea kumpenda Yesu Kristo, endelea kujivunia yeye, maana ndio mtu pekee unayepaswa kujivunia matendo yake makuu, tena alikufa na kufufuka siku ya tatu baadaye akapaa mbinguni. Akatupa msaidizi wetu ambaye ni Roho Mtakatifu, huyu ndiye anayeweza kutupa ujasiri na kutuondolea hofu.

Mshike sana Yesu Kristo yeye ndiye msaada wako wako, wakati wa tabu yako yeye ndiye msaada wako. Baba na mama watakuacha ile yeye hatakuacha kamwe, siku zote ataendelea kuwa pamoja na wewe, nyakati zote za raha na tabu yeye atakuwa na wewe.

Nikusihi sana usiache kusoma Neno la Mungu, lisha sana moyo wako Neno la Mungu, fanya hivyo uwezayo. Usijipe sababu ya kutokusoma Neno la Mungu, kama hili ni mtihani mgumu kwako, karibu sana kwenye kundi letu la kusoma Neno kila siku. Tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081.

Yesu Kristo akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com