Kujifunza kunaondoa ujinga mwingi aliokuwa nao mtu, ni kuamua yeye kuendelea kuwa mjinga baada ya kupata maarifa, ama kuamua kuwa mwerefu. Maana sio wote wanaopata maarifa huwa wanaweza kubadilika hapo hapo.
Nakiri kitabu hichi cha Wimbo Ulio Bora, kimetoa wengi kwenye giza ambalo walikuwemo. Giza hili linaweza kuwa lilifanya wengi waishi na waume/wake zao kama watu wasio mwili mmoja.
Dada yangu mmoja ambaye tupo naye group la whatsApp(Chapeo Ya Wokovu) akawa ananitania, akaniambia hichi kitabu kinakufaa sana wewe Samson, sisi wengine tunajaribu tu, akiwa ana maana kinawafaa sana wana ndoa.
Hichi kitabu hakiwafai tu wanandoa, hata wale wanaotarajia kuingia kwenye ndoa. Wanapaswa kupata elimu hii mapema, itawafaa sana baadaye. Maana wanakuwa na muda wa kutosha kujifunza wakiwa nje, na siku wanaingia ndani wanakuwa na uelewa wa kutosha.
Wakati tunaendea mwishoni mwa kitabu hichi cha Wimbo Ulio Bora, yaani nikiwa na maana kwamba, kesho tutasoma sura ya 8 na ya mwisho kabisa katika kitabu hichi cha Wimbo Ulio Bora.
Tumejifunza mengi sana, na nina imani kila mmoja aliopo humu na aliyeshiriki kusoma kitabu hichi, atakuwa ameondoka na maarifa ya kutosha. Kama nilivyotangulia kutoa tahadhari siku tunaanza kusoma hichi kitabu, nilisema hichi kitabu hakichochei ngono kwa wale ambao hawajaoa/hawajaolewa.
Hichi kitabu kinatupa mwanga kwa yale tunayopaswa kuyatenda kwa wenzi wetu, maana wapo watu wakishaokoka wanaona mambo mengine ni kama kinyaa na dhambi kwao kuyatenda.
Leo tunaenda kujifunza kwa baadhi ya viungo vinavyoweza kukuvutia kwa mke/mume wako. Na kwa wale walio na wachumba halali yaani waliotolewa au waliowatolea mahari, maana yake wanajulikana na wazazi/walezi wao, hili somo litawafaa zaidi.
Kila kiungo kina umhimu wake katika mwili wa mwanamke/mwanaume. Inategemeana na wewe kitu gani kinakuvutia kwa mke/mume wako.
Unapomsifia mke wako kwa kiungo kinachokuvutia, unamfanya ajiamini zaidi, na unamfanya akufurahie, na unamfanya ajisikie vizuri mno. Haya yote usiyafanye kinafiki yaani usimsifu kwa kitu ambacho hana, na ambacho hakikufurahishi ndani ya moyo wako.
Hebu tujifunze kwa sehemu/viungo hivi vifuatavyo;
1. KITOVU
Mpaka ukione kitovu cha mwanamke, ni mpaka awe mke wako, huwezi kuanza kumsifu mchumba wako ana kitovu kizuri.
Huo muda wa kukiona kitovu cha mchumba wako umeupata wapi? Ndio maana wadada mnatakiwa kuvaa nguo za heshima, yapo maeneo ya mwili wako mwanaume hapaswi kuyaona kabisa hadi atapokuwa mume wako halali.
Rejea: Kitovu chako ni kama bilauri iliyoviringana, Na isikose divai iliyochanganyika; Tumbo lako ni mfano wa chungu ya ngano, Iliyozungukwa na ugo wa nyinyoro. Wimbo Ulio Bora 7 :2 SUV
Msifu mke wako kama kitovu chake kinakuvutia, mpe sifa zake njema, na onyesha kufurahishwa kweli.
2. MAZIWA
Tunapopiga kelele wadada/wamama acheni kuvaa nguo zinazoacha wazi sehemu kubwa ya chakula cha watoto. Ipo maana kubwa mno, unapaswa kumfanyia hivyo mume wako, maana ni haki yake kuyaona maziwa yako.
Unapochia wazi maziwa yapo, unawapa nafasi watu wengine wayatamani, na wengine unawaingiza kuzini bila kupenda wao.
Wapo wanaume ugonjwa wao ni maziwa ya mwanamke, ndivyo Mungu alivyowaumba. Wanapoyaona unawafanya wapate wakati mgumu, sio kwamba hawajaokoka, wameokoka ila ujue ni wazima.
Wakati wengine unawaingiza kwenye majaribu kwa kuachia wazi maziwa yako, unawafanya wanaume kukushusha heshima. Kama hujaolewa unajiweka kwenye wakati mgumu kupata mwanaume anayemcha Mungu katika roho na kweli.
Na kama umeolewa unawapa nafasi watu wengine kukushusha hadhi yako ya umama. Badala ya kupata heshima, unapata dharau kwa kushindwa kujiheshimu.
Maziwa yako mwachie nafasi mume wako na mtoto wako anayenyonya, wengine hawaruhusiwi kuyaona kabisa. Uzuri wa maziwa yako anatosha kuuona mume wako.
Rejea: Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Ambao ni mapacha ya paa. Wimbo Ulio Bora 7 :3 SUV
Usiruhusu wahuni wayasifu maziwa yako kwa uzembe wako wa kuyaachia ovyo nje. Hata unaponyesha mwanao, jitahidi kujifunika na kanga, acha uzuri wa maziwa yako aone mtoto wako.
3. SHINGO NA MACHO.
Shingo ya mke wako inaweza kukupendeza macho yako hadi kugusa moyo wako, unapaswa kumweleza jinsi unavyoifurahia shingo yake.
Jinsi anavyokutazama kwa macho yake, unavyojisikia na kuyafurahia macho yake. Mweleze jinsi unayoyafurahia, atatambua kumbe unapenda macho yake.
Hii inaondoa mitego mibaya kwa watu wabaya, maana tayari atakuwa anajua yupo mtu maalum anayejua uzuri wa macho yake.
Rejea: Shingo yako ni kama huo mnara wa pembe; Macho yako kama viziwa vya Heshboni, Karibu na mlango wa Beth-rabi; Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni, Unaoelekea Dameski. Wimbo Ulio Bora 7 :4 SUV
4. KICHWA NA NYWELE.
Kichwa kimebeba nywele, wapo wanawake wamejaliwa nywele ndefu na nzuri. Huenda ikawa furaha yako kuzitazama, vizuri kumweleza jinsi unavyozifurahia nywele zake.
Kwa mwanamke inaweza kuwa kitu kizuri sana kwake, ila isije ikatokea ukamchukia kwa sababu amenyoa. Pambo moja likitoka isiwe sababu ya kuichukia nyumba yako.
Rejea: Kichwa chako juu yako ni kama Karmeli, Na nywele za kichwa chako kama urujuani, Mfalme amenaswa na mashungu yake. Wimbo Ulio Bora 7 :5 SUV
Vizuri sana kutunza nywele zako katika mazingira safi, kama huwezi kufanya hivyo, ni bora kuzinyoa kabisa ukabakisha za saizi fulani unayoweza kuitunza.
5. KIMO
Wapo wanaume wanapenda wanawake warefu na wapo wanawake wanapenda wanaume warefu. Vile vile wapo wanaume wanapenda wanawake wafupi na wapo wanawake wanapenda wanaume wafupi.
Kama unafurahia kimo cha mwenzi wako, vyema ukaonyesha kumkubali sana kuliko wanaume/wanawake wengine.
Rejea: Kimo chako kimefanana na mtende, Na maziwa yako na vichala. Wimbo Ulio Bora 7 :7 SUV
Vizuri kuoana urefu unaoendana, msipishane sana urefu, kuepuka kuogopa kutembea pamoja na mke/mume wako. Maana watu wanaweza kusema upo na mdogo wako, kumbe upo na mke/mume wako.
Bila shaka umejifunza mengi kupitia ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081