Wakati mwingine tumekuwa tunamwendea Mungu tukiwa na shida, tunakuwa siriazi kweli kumweleza shida zetu. Kufanya hivyo sio vibaya kwa upande mwingine ila kwa upande mwingine kuna shida, yaani ni sawa kumkumbuka mtu wakati wa shida ila wakati huna shida upo na mambo yako.

Kumpenda Mungu kwa misimu, yaani ukiwa muhitaji wa jambo fulani kwake ndio unakuwa bize kuutafuta uso wake ili akusaidie shida yako. Baada ya kukusaidia unageukia mambo yako, unabakia kawaida, unakuwa huna muda na Mungu.

Upendo kwa Mungu kwa mtu unaambatana na matendo, lazima mtu atatafuta kila namna kuwa na muda wa kutosha na Mungu. Uhusiano wake na Mungu unakuwa imara, anapojitoa kufanya kazi ya Mungu, anajitoa kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote,na kwa akili zake zote.

Upendo kwa Mungu unamrahishia mambo mengi sana mtu, yapo mambo bila kuomba, Mungu anakuwa anafanya tu kwake. Anakuwa anashangaa tu anapokea mambo mazuri katika maisha yake bila kujua nini kimetokea kwake.

Kumpenda Mungu ni amri kuu, ikiwa ni amri kuu, na ukashindwa kuifuata au kuitenda, unafikiri nini kitafuata? maana ni amri iliyo kuu. Uwe na uhakika hakuna usalama katika maisha yako, kwa kutompenda Mungu.

Rejea:- Akawaambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. MT. 22:37-38 SUV.

Upendo sio maneno matupu, huwezi kusema unampenda Mungu alafu huna muda naye, huna ibada naye, unakuwa bize tu na mambo yako. Hata kule kutafakari neno lake huna muda huo, moyoni mwako hukumbuki lini ulitafakari juu ya Mungu zaidi upo bize na maisha yako.

Kumpenda kwetu Mungu kunapaswa kuakisi katika matendo, maana kama unampenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na akili zako zote. Lazima ujipambanue na watu wengine ambao wanaishi katika ukaiwada au mazoea.

Maono ya mtu kutimia ni vile uhusiano wake na Mungu upo vizuri, maana hadi kufikia maono yako au ndoto yako ni mchakato mrefu mno. Mchakato ambao unamhitaji sana Mungu akusaidie uweze kufikia hatima yako njema.

Kama umeamua kuokoka, maanisha kweli, kumpenda Mungu kuwe ndio kunatawala moyo wako, hiyo itakufanya kuwapenda na wengine. Ikiwa moyoni hakuna kumpenda Mungu, ujue kumpenda mwingine ni ngumu kwako. Maana upendo wa kweli unatokana na Mungu mwenyewe.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.

+255759808081