Wengi sio wageni na neno hili ushauri, ni neno ambalo tunalisikia kila mara, haitoshi tu kulisikia, inawezekana kabisa tumewahi kutoa Ushauri, au kupewa ushauri na wengine.

Inawezekana ni wazazi wako, au ndugu zako, au jamaa zako, au rafiki zako, au viongozi wako, walikupa ushauri ambao ulikuwa unauhitaji.

Kuna ushauri wa kuomba wewe, unaenda kwa mtu au watu unaoona wanaweza kukusaidia mawazo mazuri juu ya jambo fulani linalokupa changamoto katika maisha yako.

Na kuna ushauri ambao watu wanakupa bila kuwaomba wakushauri, wanakukalisha chini na kuanza kukushauri juu ya jambo fulani. Inawezekana kabisa kitu wanachokushauri wamekiona hakiendi sawa kwako, au wameona wasipokuambia unaweza usiende vizuri kama inavyotakiwa.

Tumeona aina hizo mbili za ushauri, sasa niongelee ushauri wa kuomba wewe. Unakutana na jambo gumu na moyo wako unakutuma kwenda kwa watu fulani kuomba ushauri kwao.

Unakuwa na uhakika ushauri wa hao watu unaweza kukusaidia, inakuwa hivyo kutokana na vile walivyo hao. Ni watu wanaoelewa mambo mengi sana na wanamcha Mungu katika roho na kweli, wakikushauri jambo wanakushauri vizuri.

Naomba unielewe hapa, sio kila ushauri unapaswa kufuatwa, wakati mwingine usipokuwa makini hata wale unaowaamini wanaweza kukushauri vibaya na ukamkosea Mungu wako.

Shida inakuja pale unapoenda mahali kuomba ushauri, au unapoita watu wakushauri, na hao watu wanakushauri kwa hekima vile uliomba wakusaidie.

Kama tunavyoona kwa Rehoboamu alitaka ushauri wa wazee juu ya jambo lililokuwa limemtatiza akashindwa afanye nini.

Rejea: Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? 1 FAL. 12:6 SUV.

Baada ya wazee hao kuambiwa hivyo na wao hakuwa wazito kusema kile ambacho walikuwa wanaona ni chema kwa Rehoboamu. Wakamwambiaje sasa Rehoboamu?

Rejea: Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima. 1 FAL. 12:7 SUV.

Nikukumbushe tu kuwa sababu ya Rehoboamu kutaka ushauri ilikuja pale alipoombwa jambo na Yeroboamu na jamii yote ya Israel. Waliomba nini kwa Rehoboamu? Unaweza ukajiuliza hivyo, Rejea mstari huu hapa chini;

Rejea: Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. 1 FAL. 12:4 SUV.

Hiyo ndio sababu iliyomfanya Rehoboamu kutaka ushauri wa wazee, na wazee hao hawakuwa na uzito katika hilo la kumpa ushauri. Walimpa ushauri mzuri sana ila akaupuuza.

Rejea: Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake. 1 FAL. 12:8 SUV.

Alivyoukataa ushauri wa wazee hao, hakuishia hapo, Biblia inatuambia akataka ushauri kwa vijana. Sijui kama tupo pamoja hapa, yaani ule ushauri wa kwanza ambao ulikuwa mzuri akauacha na kutafuta mwingine.

Na wale vijana hawakuwa na hiana, wakamshauri ushauri ambao na yeye Rehoboamu aliona ni ushauri sahihi. Kumbe haukuwa ushauri sahihi, kwanini nasema hivyo? Ulikuwa ni ushauri wa utawala wa mabavu.

Rejea: Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa; akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. 1 FAL. 12:13‭-‬14 SUV.

Hii inatufundisha kwamba sisi vijana tunaweza kupewa ushauri wenye hekima na wazee, tukaona tukapate na wa vijana wenzetu kama ilivyokuwa kwa Rehoboamu. Badala yake tunapewa ushauri mbaya.

Tujifunze hili kama vijana viongozi, tunapopewa ushauri wa hekima tufuate na kuufanyia kazi. Maana una matokeo mazuri katika uongozi wetu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081