Mtu yeyote mwenye Roho Mtakatifu ndani yake, na aliyejaa Neno la Mungu ndani yake, anapokutana na jambo ambalo lipo kinyume na Neno la Mungu. Mtu yule lazima atachukizwa sana na kitendo hicho.

Ninyi kama wenyeji mnaweza kukaa tu na kuona ni jambo zuri kufanya hivyo, ila anapokuja mtu mwingine mgeni anayemjua Mungu vizuri kupitia Neno lake. Atajua kabisa kuna mahali hampo sawa, kutokana na mwenendo mnaoenda nao.

Mtu huyo anapopata nafasi ya kuzungumza, anaweza asizuie hisia zake kutokana na mwenendo mbaya wa kanisa au kundi fulani. Kueleza ukweli anaweza kueleza, ila anaweza asieleweke haraka.

Maana mtu aliyezoea kufanya jambo fulani, hata kama ni baya sana, kumwondoa kwenye imani yake inahitaji Neema ya Mungu. Wapo watakuelewa, na wapo hawatakuelewa kabisa, zaidi watakuchukia tu.

Kwahiyo ukiwa kama mkristo ambaye una wajibu wa kuhubiri habari njema za Yesu Kristo, unapofika mahali ukachukizwa na jambo fulani. Ambalo unaona kabisa linafanywa kinyume na Neno la Mungu, usijione ni mchanga kiroho ndio maana unachukizwa na mambo kama hayo.

Hili la kuchukizwa na jambo, tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Paulo, alifika mahali akakuta watu wanaabudu sanamu. Hicho kitu kilimfanya Paulo achukie sana.

Rejea: Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake. MDO 17:16 SUV.

Ndugu, kuchukizwa na jambo ukiwa kama mtu uliyeokoka sawasawa, sio jambo ambalo ni baya sana kwako. Ni jambo ambalo linaweza kuwapata watu wa Mungu waliojaa Roho Mtakatifu ndani yao.

Unapochukizwa na jambo lolote ni rahisi sana kwako kukemea, maana litakuwa ni jambo ambalo lipo ndani ya moyo wako.

Usisite kusema pale unapoona watu wanaenda kinyume na maagizo ya Mungu, watu watakuchukia na kukuona sio mtu mzuri kwao. Hilo lisikutishe na kujiona labda umekosea, hujakosea kitu bali umetii agizo la Roho Mtakatifu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com