Haleluya,

Kuna wakati unaweza kusoma biblia na kuanza kujiuliza mengi sana, kuna tabia tunaweza kusema ni mpya au tunaweza kusema labda mtu amejiundia tu kumbe zilikuwepo tangu zamani.

Tabia ya kukonyezana kumbe ipo ndani ya maandiko matakatifu, kumbe haka ka tabia kanaonekana ni hatari sana kwa watumiaji wake. Kwa upande mwingine kanaweza kuwa kazuri, ila hapa naenda kuzungumzia zaidi madhara yake.

Kukonyezana kwa tafsiri nyingine isiyo rasmi sana tunaweza kusema ni kupeana/kupewa ishara fulani anayotoa mtu kufikishia ujumbe fulani aliokusudia ukufikie/umfikie mhusika. Ishara hii hutumika sana na viungo vya mwili hasa macho.

Hasa ukikutana na kahaba, hutumia sana macho yake kukonyeza, na vidole vyake huashiria jambo fulani hata bila kutoa sauti.

Ukikutana na majambazi wanaofanya ualifu. Mara nyingi hutumia ishara za mikono/vidole kunena au macho yao kukonyezana.

Viungo vyetu vya mwili ni vizuri sana, ila watu wasiomjua Mungu huvitumia vibaya kumzalia shetani matunda. Kama mtu anaweza kutumia vidole vyake kumtenda Mungu dhambi ujue ni hatari sana.

Kama kope za macho zinaweza kumwingiza mtu kwenye uzinzi/uasherati, ujue sio jambo la kupuuza kabisa. Wengi wameingia kwenye mtego huu, utasikia niliona ananiangalia sana nikajua amenipenda, kumbe hajapendwa ametamaniwa.

Kwa namna moja ama nyingine umewahi kuona mtu na mke wake wamekaa meza moja ya chakula, wanakula labda na dada wa kazi au dada wa mke wake au rafiki wa mke wake. Mume wake wanakuwa wanatumia miguu yao chini kwa chini kufikishiana ujumbe mbaya wa kwenda kufanya uovu.

Wakati mwingine wanaweza kuwa hawana mazoea kabisa, ila akatokea mmoja wapo amemtamani mwinzie, anatumia miguu yake kunena na shemeji yake au kijakazi wake mbele ya mwenzi wake.

Naeleza namna kukonyezana inavyokuwa, usije ukafikiri naeleza vitu ambavyo havipo kwenye maandiko matakatifu. Najaribu kukufafanulia zaidi uweze kuelewa mitego inayowasababisha watu wengi waingie bila kujielewa.

Rejea: Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu. Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake. Mithali 6:12_13 SUV

Umeona hapo, macho yanakonyeza, miguu inanena kama unavyonena ulimi, na vidole navyo huashiria jambo. Unaweza kuona ushirika huu wa viungo vya mwili ulivyo mkubwa hapo, ushirika unavyompelekea mtu amtende Mungu dhambi.

Hebu tujiepushe na haya, kukonyeza sio neno jipya la mtaani, ni neno lililoandikwa kwenye Biblia takatifu. Usije kufikiri ni maneno ya kihuni tu mtaani, haya ni maneno hai tunayoyaona leo kwenye maisha yetu ya kila siku.

Mungu akubariki.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081