Mtumishi wa Mungu anapokaa katika nafasi yake, anapofundisha maneno ya Mungu, anapohubiri habari njema za Kristo, ni sawa na Mungu mwenyewe amesema.

Mungu anawatumia watumishi wake kufikisha ujumbe unaopaswa kuwafikia watu wake, unapokataa kumsikiliza kile anasema, unapokataa kumtii kwa kile anakuamru ufanye. Uwe na uhakika umemkataa Mungu mwenyewe.

Kama huna heshima kwa watumishi wa Mungu, huwezi kumweshimu Mungu usiyemwona kwa macho ya nyama. Ukisema huwezi kumweshimu mwanadamu mwenzako, utamweshimu tu Mungu, utakuwa unajidanganya mwenyewe.

Mchungaji wa kweli, mtume wa kweli, nabii wa kweli, mwinjilisti wa kweli, mwalimu wa kweli, huyu ni mjumbe halisi wa Mungu. Anapozungumza jambo linalohusu maisha yako, uwe na uhakika Mungu amesema kupitia kinywa cha mtumishi wake.

Kumsikiliza mtumishi wa Mungu anayehubiri habari njema za ufalme wa Mungu, anayefundisha mafundisho mbalimbali ya Neno la Mungu. Ni sawa na umemsikiliza Mungu mwenyewe.

Neno la Mungu lipo wazi kabisa kuhusu hili ninalokuambia hapa, usifikiri ni maneno tu ya kuokoteza mtaani. Hili ni Neno la Mungu lililo na pumzi ya Mungu.

Rejea: Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. LK. 10:16 SUV.

Tena Yesu anasema, wale wanaowakataa watumishi wa Mungu, ni sawa na kumkataa Yesu mwenyewe. Ili ukubalike vizuri mbele za Mungu, unapaswa kujifunza hili vizuri.

Ukiwa kama mtumishi unayetumika shambani mwa Bwana, jua umebeba dhamana kubwa sana juu ya watu wengine. Neno lako ni sauti ya Mungu imezungumza kupitia kinywa chako.

Maneno yetu yawe yenye kuponya, kukemea, kuonya, kukanya, kufundisha, ili wale wanaotusikia waweze kubadili tabia mbaya katika maisha yao.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com