Ukisoma kichwa cha somo hapo juu unaweza ukapata picha nyingi sana kutokana na wakati tulionao sasa wa watumishi wanaotumia vibaya jina la Yesu.

Huenda hata kuingia kuanza kusoma somo hili umejisukuma tu kwa nguvu ila ndani yako una mambo mengi ambayo yanakutatiza, hasa upande wa utoaji wa sadaka.

Somo hili halitakuambia utoe ila litakufundisha kibiblia vile matoleo yalitolewa kwa ajili ya kazi ya Bwana.

Tunaweza kwenda pamoja katika somo hili, hadi unafika mwisho wa somo hili utakuwa umejifunza kitu ambacho kitakusaidia katika maisha yako ndani ya Yesu.

Tumeona kwenye makanisa yetu wakisema tunataka tumnunulie mchungaji wetu gari zuri, wengine pikipiki, kutokana na uwezo walionao washirika.

Hili huenda linawaletea wengine shida kwenye mioyo yao, huenda sio washirika tu, hata wachungaji wenyewe huenda wanapata shida kwenye mioyo yao.

Kwa kufikiri wanamkosea Mungu kwa kuruhusu kununuliwa gari au pikipiki au usafiri wowote ule wa kuwasaidia katika utumishi wao.

Kabla sijakuambia ni sahihi ama sio sahihi, labda nikuambie tu kwamba hili jambo halikuanza zama hizi. Tangu agano la kale hili jambo lilikuwepo kwa watumishi wa Mungu waliokuwa wanamtumikia.

Rejea: Nao wakamletea BWANA matoleo yao, magari sita yenye mafuniko juu, na ng’ombe kumi na wawili; gari moja kwa wakuu wawili wawili, na ng’ombe mmoja kwa kila mkuu; nao wakayasongeza hapo mbele ya maskani. HES. 7:3 SUV.

Hapa inasema wakamtolea Bwana matoleo yao, ambayo ni magari kadhaa yaliyotajwa idadi yao kwenye hilo andiko, sio magari haya ya kipindi hichi. Hayo yalikuwa magari ya kipindi hicho.

Kwanini walipewa magari haya, walipewa kwa ajili utumishi, kurahisisha kazi ya utumishi, mtumishi anapotaka kwenda mahali kwa ajili ya kazi iwe rahisi kwake.

Hili limewekwa wazi katika mstari huu nitakaoenda kukushirikisha hapa chini, utaona ni jinsi gani usafiri huu wa magari ulitolewa kwa ajili ya nini.

Rejea: Pokea mikononi mwao, ili kwamba viwe vya kutumiwa katika utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawapa Walawi vitu hivyo, kila mtu utampa kama utumishi wake ulivyo. HES. 7:5 SUV.

Sijui kama umeelewa hilo andiko, tunazungumza matoleo ya Bwana yaliyotolewa kwa ajili ya kazi yake. Na yakatolewa maelezo ya jinsi ya kumgawia kila mtumishi kutokana na majukumu yake.

Utakuwa umeona hili jambo la kusisitizana kununua usafiri wa mchungaji litakuwa sio jambo linaloanza nyakati hizi. Hili jambo lilikuwepo tangu kipindi cha Musa, unapoliona katika kipindi chetu hupaswi kutayarika.

Ikiwa wapo waliotoa kwa ajili ya kazi ya Bwana, inapotokea kanisani kwako kwa mtumishi wa Mungu wa kweli. Hupaswi kushangaa kabisa, hili lilikuwepo tangu zamani.

Sio sheria kumnunulia mchungaji wako usafiri ila fahamu kwamba tangu mwanzo jambo hili lilikuwepo. Ikiwa lilikuwepo na sisi tunasoma maandiko matakatifu, unapaswa kuelewa hili.

Tena unapaswa kuelewa haya yanayotokea kanisani kwako yalishatokea, haukuwa usafiri wa nyakati za leo ila tumejifunza jambo la muhimu sana katika nyakati tulizonazo leo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081