Hili naliandika kwa ujasiri mkubwa kabisa, na nisipokuambia wewe kama rafiki yangu nitakuwa sijatenda haki kwako.

Kuna watu wapo makanisani leo hii wanamwabudu Mungu, na wengine wanahudumu madhabahuni lakini ni wahuni tu wa kawaida kabisa kama wahuni wengine wasiomjua Kristo.

Wanafikiri wanamficha mchungaji na washirika wengine lakini mwenye kutoa hukumu uende motoni au peponi hawawezi kumficha.

Leo hii wazinzi wamejaa makanisani, unaweza wewe unayesoma ujumbe huu na ni muumini wa dhehebu lako utaniunga mkono kwa hili maana kwa namna moja au nyingine utakuwa unashuhudia uchafu huu kwa watu.

Leo hii tumejaza wamama/wadada/wababa wanaovuruga ndoa za watu wengine, mtu yupo tayari kutembea na mke/mume wa mwenzake akijua kabisa ni wa fulani. Bora angekuwa anajisikia vibaya kwa hili, hajatosheka kutembea na mume/mke wa mwenzake anarudi tena kushirikiana kumharibu mke/mume wa mwenzake kwa maneno mabaya ya kumuumiza, kujionyesha yeye ndiye anayemmiliki huyo mwanaume/mwanamke.

Kijana wa kiume anaenda ibadani si kwa kusikiliza neno la Mungu bali kuangalia mabinti, na mabinti nao hawaendi ibadani kwa nia ya kusikiliza neno bali kuonyesha wenzao leo wametokaje na mtindo mpya wa nguo.

Inaumiza, inakera, na mbaya zaidi mama wa watu kuacha kuhudumiwa na mume wake kwa sababu yako wewe, ni mbaya sana baba wa watu hapati mahitaji mhimu kwa mke wake, sababu yako wewe mama/dada umemshikilia mume wake.

Ukiwa umevunja ndoa ya watu, ama umeisambaratisha kwa juhudi zako wewe kumlaghai huyo mjinga mwenzio, neno la Mungu linasema hivi;

atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.
1 Yohana 3 :8

Hebu tumwogope Mungu ndugu zangu, maana tunapoelekea haina tofauti na Sodoma na Gomora, ikiwa mtu anaishi ndani na mume/mke wa mwenzake pasipo hofu yeyote, unafikiri hapo kuna nini tena.

Najua utasema hivi we Samson umeona dhambi pekee ni ya uzinzi/uasherati tu?, upo sahihi kuwaza hivyo kwa mtazamo wako, ila ninachoandika hapa ndio ujumbe niliopanga nikuletee siku ya leo.

Kabla Mungu hajaamua kuonyesha ulimwengu mzima tabia yako chafu, nakusihi Uache tabia hii mbaya, usipende kuitwa jina mkristo lakini ndani yako hauna Kristo.

Samson Ernest.

+255759808081.