Sio jambo geni kuona mtu fulani aliyekuwa amefanikiwa sana kwenye biashara zake, au alikuwa na cheo kikubwa. Alivyoondoka kwenye nafasi hiyo, na akaona anguko lake hilo ni aibu kwake kwa wale aliokuwa anafahamiana nao.

Wengi wamechukua maamuzi ambayo wangekuwa na Roho Mtakatifu ndani yao wasingefanya hivyo.

Kinachowafanya watu wengi waliofanikiwa kwenye nafasi fulani kuchukua maamuzi ya kujiua. Ni kule kukwepa aibu ya watu wengine wakiwa kwenye hali ya kukosa.

Hasa watu wanaochukua maamuzi hayo ni wale ambao hawana Yesu mioyoni mwao.

Wale ambao hawajampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Ama walishampokea ila wakafika mahali wakarudi nyuma.

Wanapopatwa na shida ngumu, mfano; alikuwa na mali nyingi. Anapofilisika au anapoendea kufilisika, anaona aibu inayokuja baada ya kufilisika ni kubwa anaamua kuchukua maamuzi ya kujiua.

Hili tunaliona kwa Sauli, akiwa kwenye vita, alivyoona amezidiwa na jeshi lake, na watoto wake kuawawa. Hakutaka kuja kuawawa na Wafilisti, aliamua kujiua mwenyewe.

Rejea: Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.1 SAM. 31:4 SUV.

Hata leo haya mambo yapo, hasa wale ambao tumaini la Kristo halimo ndani yao. Ambao maisha yao waliamua kuishi bila kumpokea Bwana Yesu.

Inawezekana wapo wanaonekana kwa macho maisha yao yanamtegemea Kristo, lakini yapo maisha mengine ambayo wanategemea msaada kutoka kwa miungu mingine.

Kujiepusha na hili jambo la kukwepa aibu, na kuamua kujichukulia maamuzi ya kujiua. Au kumshawishi mtu mwingine akuue, maisha yako yote unapaswa kumkabidhi Yesu Kristo.

Biashara zako, kazi yako, haipaswi kukutenganisha na Mungu wako. Haijalishi utafanikiwa kiasi gani, Mungu anapaswa kuwa kipaumbele chako cha kwanza katika maisha yako.

Utajiepusha na aibu ambayo ingekuwa chanzo cha wewe kujiua kwa sumu, au kujipiga  risasi, au kujinyonga na kamba.

Ili tu kukwepa aibu ya ndugu zako, marafiki zako, majirani zako, na jamii yote inayokuzunguka. Maana ilikufahamu ulivyokuwa na uwezo mkubwa.

Na wakati mwingine uhusiano wako na wao hukuwa mzuri kabisa, unafikiri vile watakusema unaona bora ujiue kukwepa fedha hiyo.

Je, ya nini yakutokee hayo kama Sauli? Usikubali kupoteza uhusiano wako na Mungu kama ilivyokuwa kwa Sauli.

Hakikisha uhusiano wako na Mungu upo vizuri siku zote, imarisha mahusiano yako na Mungu siku zote za maisha yako.

Mungu akusaidie.
Samson Ernest
+255 759 80 80 81