Kipindi cha Goliath wa Gati alivyokuwa analitukana taifa la Israel, siku Daudi anajitokeza kupambana na Goliath. Baada ya kumpiga Goliath, jeshi lote la Walifilisti lilikimbia.
Kilichowakimbiza Wafilisti ni nini? Ni baada ya kuona Goliath amepigwa na Daudi, wakaona kama jitu kubwa lenye nguvu nyingi. Jitu lililokuwa linaogopwa sana na taifa la Israel, wakaona limeanguka chini, wakaona wao si lolote.
Wakati mwingine sio lazima kushindana sana na adui yako, angalia adui yako anapata nguvu wapi au anapewa nguvu na nani za kukusumbua wewe.
Ukishapata chanzo cha nguvu zinazompa kiburi, shughulika nazo, utakapovunja hizo nguvu zake katika jina la Yesu Kristo. Utaona hata wale maadui zako wadogo wadogo watakimbia wenyewe.
Usitishwe na idadi kubwa ya maadui zako, angalia mkubwa wao aliyejuu ya wote ni nani, kisha shughulika na huyo. Ukishampiga aliye na nguvu kuliko wote, utaona wengine wakijawa na hofu kisha kukimbia wenyewe.
Hili nakueleza katika mazingira ya kawaida kabisa, Unaweza kusumbuliwa sana na watu kadhaa ambao nia yao ni mbaya kwako. Ukishaona hivyo usihangaike na hao wote wala usitishwe na wingi wao, nenda mbele za Mungu.
Mweleze Mungu shida yako, Mungu atampiga aliyemkubwa na wengine wanaomfuata huyo mkubwa watakimbia. Inawezekana kabisa walikuwa hawajuani kama wanataka kukuangusha wewe, wataposikia kuna mtu amepigwa pigo lisilo la kawaida. Na mtu huyo anafahamika ana nguvu za kutosha, bila kuhoji watakimbia wenyewe.
Haya tunajifunza kupitia Neno la Mungu, ndio maana nilikuanza na mfano wa Goliath na Daudi. Daudi hakushughulika na Wafilisti wote, Daudi alishughulika na Goliath tu.
Ipo miji mingi ilikuwa inasumbua Israel, Mungu aliamua kuupiga mji mmoja tu ambao ni Tiro. Mingine baada ya kuona hicho kipigo cha Tiro, ilijawa na hofu na kuogopa.
Rejea: Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto. Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu. ZEK. 9:4-5 SUV.
Umeona hapo, baada ya mji wa Tiro Mungu kuahidi kuuteketeza/kuupiga na kuondolewa mali zake zote, miji mingine kama Ashkeloni, Gaza, na Ekroni, itajawa na taharuki kubwa.
Bwana anajua nguvu ya adui zako zipo wapi, kuna mtu anakunyanyasa kwa sababu ya cheo chake. Mtu mwingine anakunyanyasa kutokana na uwezo wake wa kifedha, mwingine anakusumbua kwa sababu ya nguvu za giza.
Vita vyetu si vya damu na nyama, huwezi kusema ngoja nikamfanye kitu kibaya aache kuringa. Hilo sio jukumu lako, Mungu wako anajua nguvu za adui zako zipo wapi, pale zilipo nguvu za adui zako, atampiga yeye.
Akishampiga mmoja, wote waliokuwa wanakusumbua watakimbia wenyewe. Hii ni kanuni ya kiMungu, kuna maadui huenda usiwajue kama wanakunyemelea wakumalize ila kupitia kupigwa kwa adui yako mmoja unayemfahamu, wengine wote watakimbia wenyewe.
Mtegemee Mungu katika maisha yako yote, tena hakikisha Neno la Mungu halipungui kwako. Vitu kama hivi huwezi kuvifahamu kama husomi Neno la Mungu, kusoma kwako Neno la Mungu kunakupa kufahamu wa haya yote.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.