Mwl: Kashai M.

Yoh 3:16
16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Bwana Yesu Apewe sifa mpendwa msomaji wangu!

Leo acha tupate dakika chache tujifunze kwa habari ya utoaji uletao baraka malangoni petu.

Kila kitu kina kanuni zake na ni wachache wawezao kutafuta na kujua kanuni za kila jambo! Mara nyingi huwa hatuna muda wa kutafuta undani wa kitu tunachokitafuta kinapatikanaje?

Kuna maneno mengi huwa yanasemwa kuhusiana na matoleo hasa yale yaitwayo sadaka. Watu wengi wameyapotosha maandiko na kuwafundisha wengine mabaya au vibaya ila ukweli huwa unabaki palepale.

Kwa kawaida kabisa hii haihitaji tafsiri ya rohoni Wala ya elimu ya chuo kwamba kama mtu hajawai kulima shamba ni vigumu kwake kupata mavuno labda awe mwizi, huyo atavuna asipopanda.

Leo nataka nikueleze kwamba Jambo la utoaji ni la kiroho na la kimwili pia na vyote ni sahihi. Watu wengi wamesema matoleo ya kanisani siyo sahihi na wale watoao basi wanawatajirisha wachungaji.

Lakini ukweli ni kwamba hauwezi kuvuna usipopanda, tumesoma mstari mmoja hapo juu ambao ni mstari maarufu Sana kwenye biblia na ni mwepesi kufahamika unasema kwamba Mungu aliupenda ulimwengu..

Kwa hiyo kanuni mojawapo ya utoaji sadaka, itaambatana na upendo na pasipo kusukumwa na upendo basi hautaweza kutoa chochote mbele za Mungu.

Maandiko yanatuonyesha mtoaji wa kwanza ni Mungu mwenyewe na alitoa mbegu moja tu iitwayo Yesu Mwanae wa pekee mbegu akaipanda udongoni na Kisha ikaota ikakua ikazaa watoto wengi wa kutosha leo hii Mungu anaitwa baba ulimwengu pote.

Hii haikuwa hivyo tangu Adam bali katika Kristo Yesu Mungu wetu ndiye Baba yetu wa Mbinguni.
Kwa hiyo ishara mojawapo itakayoonyesha kwamba wewe una upendo ni vile unavyotoa.

Hata kwenye mambo ya kawaida unapopenda kitu au mtu itakupasa utoe. Ukiipenda nguo basi utatoa pesa ili uipate la sivyo hautaipata

Mungu aliupenda ulimwengu huu tunaoukaa ndipo akamtoa mwanawe wa pekee. Kwa hiyo unaweza kuuona msukumo wa upendo ndani ya moyo wa Mungu kwamba alipoupenda ulimwengu Akamtoa Yesu kama chachu ya uzima

Huwezi kusema unapenda afu unakataa kutoa hiyo itakuwa haijakaa sawasawa! Ukipenda lazima utatoa na hicho ndicho alichokifanya Mungu kwamba alipopenda akatoa.

Turudi kwa Ibrahim kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu alibidi amtoe Isaka na alipomtoa ndipo Mungu akasema “Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

Pale anaposema *unamcha Mungu anamanisha *unampenda Mungu ndo maana hukunizuilia mwanao*
Unapopenda huwezi kuzuia ukipenda utaachilia yaani utatoa Wala hutazuia.

Huwezi ukaitenga injili na kutoa kwa sababu Injili imezaliwa na kutoa yaani Kama Mungu asingemtoa Yesu wala tusingehubiri chochote kwa watu lakini Leo tunamhubiri Kristo aliye hai.

Huwezi kusema unampenda Mungu alafu unachukia kutoa sadaka hapana upendo unakusukuma kutoa wala siyo kuzuia kwa hiyo ukitaka kuonyesha umependa au unapenda Jambo lolote lazima gharama yake ni kutoa.

Injili ilisimama kwenye mhimili wa kutoa tangu Mbinguni hata Sasa kwamba Mungu alipopenda Akamtoa Mwanae Sasa wewe leo unaposema unampenda Mungu Kisha ukazuia sadaka una upendo wa namna gani?

Maandiko yanasema Upendo haupungui neno wakati wowote unapopenda na bado huwezi kutoa bado kuna kitu kinapungua kwako kwenye alama za upendo.

Kutoa ni upendo kwani kupenda huwa ni hiari kwa hiyo tunatoa kwa hiari yaani tunatoa kwa upendo siyo kulazimishwa maana upendo haulazimishwi upendo ni hiari acha tusome *”Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, *kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao“*; (2Kor 8:3)

Kwamba kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao hapa ingesema kwa upendo wao wenyewe walitoa vitu vyao yaani walisukumwa na upendo wakafanya tendo hilo la utoaji.

Yaani siyo kwamba kutoa mpaka uwe navyo vingi bali ukiwa na moyo wa upendo hata kile ulichokitoa kama ni kidogo kitaleta baraka kwako na kwa wengine pia
12 Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.(2Kor 8:12)

Kama utatoa kwa moyo wa kupenda yaani moyo wa hiari utakubaliwa na Mungu kwa sadaka hiyo uliyotoa au uliyonayo ko unaweza kuona jinsi Mungu anavyothamini utoaji kwamba hata kile kidogo alicho nacho akikitoa kwa upendo kinapata kibali.

Napenda kusema kuwa kutoa siyo mpaka uwe na vitu vingi bali vile vichache Kama vile Ibrahim hakuwa na watoto wengi bali Isaka lakini alitakiwa kumtoa na akamtoa na Mungu akambariki, Mungu mwenyewe alimtoa Yesu mwana wa pekee maanake alikuwa naye mmoja.

Na alipomtoa Yesu alipata watoto wengi wakike na wakiume walioko duniani na huko Mbinguni. Nakusisitiza kwamba heshimu Sana nafasi hii ambayo shetani anawazuia wengi wasiuone uzuri wake japo kwa shetani kutoa ni lazima wanatoa hadi watoto wao au wazazi wao na bado watakufa motoni.

NAKUKARIBISHA UUONYESHE UPENDO WAKO KWA MUNGU WAKO AMBAYE YEYE ALIPOKUPENDA WEWE ALIMTOA YESU WEWE UNAMPENDA UMETOA NINI

By Kashaimedard@gmail.com
Neno la Mungu ni Taa