Kuna mahali mtu anaweza akafika akawa na mawazo fulani ya kumuumiza moyo wake.

Mawazo aliyonayo yanakuwa yamesababishwa na mambo magumu yaliyo mbele yake.

Akitazama jambo fulani lilivyokaa au lilivyomtokea, linakuwa linampa wasiwasi mwingi.

Ikitokea watu wa pembeni wakaonyesha kushtushwa na hicho kitu. Hofu au wasiwasi wa yule mtu unakuwa mkubwa zaidi.

Dawa ya mtu anapokuwa na wasiwasi juu ya jambo fulani lenye utata kwake. Anapaswa kuondolewa huo wasiwasi kwa kupewa maelezo ya kina na sahihi.

Utaona huo wasiwasi wake unaondoka kabisa kwa huyo mtu.

Hili tunajifunza kwa Manoa, mke wake alimsaidia kumwondoa kwenye hofu.

Rejea: Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. Lakini mkewe akamwambia, Kama BWANA angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. AMU. 13:22‭-‬23 SUV.

Kuwa na maarifa sahihi ya neno la Mungu, au kuwa na maarifa sahihi ya jambo fulani ni muhimu sana kwa mkristo.

Inawezekana kabisa ukawa kwenye utata mkubwa kuhusu jambo fulani ila ukipata rafiki mwenye ufahamu wa hilo jambo utaondoka kwenye hiyo hofu.

Wapo watu wenye hoja za kukusaidia kuondoka kwenye hali inayokutia wasiwasi.

Unaweza kukutana na mtu ukamweleza jambo lako, vile anakujibu ni kwa njia nyepesi sana na ikakusaidia.

Mungu akukutanishe na mtumishi wake wa kukuondoa kwenye hali inayokutia wasiwasi, au akukumbushe neno lake la kukuondoa kwenye wasiwasi.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.