“Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye”, Mwa 31:19 SUV.

Raheli kuiba vinyago vya baba yake Yakobo, alafu wakati wa ukaguzi akamdanganya baba yake asivione ili aendelee kuwa navyo yeye.

“Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago”, Mwa 31:35 SUV.

Kutokana na uvumbuzi wa mambo ya kale katika maeneo hayo ilionyesha kwamba kumiliki vinyago vya mzazi ilikuwa inakuhakikishia kuja kumiliki mara mbili mali za baba pale atakapokufa.

Kutokana na mjadala waliokuwa nao Lea na Raheli inaonyesha wazi waliona wamedhulumiwa urithi wao na baba yao.

“Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?”, Mwa 31:15 SUV.

Raheli akaona avichukue vile vinyago vya baba yake si kwa ajili ya kuviabudu au kuvifanya mungu wake, bali ilikuwa kwa ajili ya kuja kufaidika na fedha za baba yake.

Malengo yake hayakufanikiwa kama alivyopanga, baadaye tunaona Yakobo alikuja kutoa amri ya kuvitekeza vinyago vyote na aina zote za miungu migeni iliyokuwa kwenye nyumba yake.

“Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu”, Mwa 35:2 SUV.

Hii inatufundisha kwamba tunaweza tukawa na vitu ambavyo sio sahihi mbele za Mungu kwa kigezo cha kuja kupata kitu fulani.

Vitu hivyo vinaweza vikatumika kuondoa uwepo wa Mungu katika maisha yetu, hata kama nia yetu  sio kuviabudu bado tutakuwa na kitu ambacho ni chukizo mbele za Mungu.

Tunapaswa kuondoa kila kitu katika maisha yetu tunapoamua kuokoka, vile vitu ambavyo tunavyo kwa kufikiri ni ulinzi wetu au ni mila zetu kuwa navyo tunapaswa kuachana navyo kabisa.

Tunaweza tukawa watu wazuri tu na kupata vyote tunavyovihitaji mbele za Mungu bila kuwa na miungu mingine ya mababu na bibi zetu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081