Haleluya,

Heri ukawa na neno la kujitetea mbele za washtaki wako, hata kama hutowajibu hoja zao kwa maneno ya kinywa chako. Ndani ya moyo wako uwe na jibu ambalo litakupa nguvu za kuendelea kuishi maisha matakatifu, yasiyo na maswali mengi kwa wale wasiomwamini Kristo.

Zipo kweli Nyakati tunapitia, ambazo hizo nyakati wakitutazama wale ambao wanatujua sisi ni wakristo. Kuna maswali mengi huwa wanapata wanapoona tunanyanyaswa na jambo fulani ambalo kwa akili ya kibinadamu hatukustahili kuteswa na jambo dogo kama lile.

Kweli kabisa yapo maswali mengi juu yetu hasa sisi tuliokoka, maswali haya yanatokana na kwanini huyu mkristo apitie hali hii ikiwa yeye ana Mungu wa kweli ndani yake.

Tunawaona wanawake wengi ndani ya biblia waliokosa watoto katika ujana wao, walipokea shutuma nyingi sana. Moja ya wanawake hao alikuwa Raheli mke wake na Yakobo, wakati Lea anaendelea kuzaa watoto akifikiri ataongeza upendo kwa Yakobo, Raheli hakuwa na mtoto hata mmoja.

Hivi unafikiri wakati Sara mke wake na IBRAHIM, kabla hajapata mtoto wake Isaka maneno mangapi yalisemwa juu yake. Kama tunavyojua wanadamu tulivyojaliwa maneno mengi na kujiona tunaelewa sana mambo ya watu, huyu mama lazima kuna vimaneno visivyo vizuri vilikuwa vinamfikia.

Hivi unafikiri Elisabeth mke wake Zakaria ambaye ni mama yake na Yohana mbatizaji, mpaka anafika umri ule akiwa hana mtoto mpaka kuja kupata fursa ya kumpata Yohana. Unafikiri maneno mangapi aliyapata kutoka kwa ndugu wa mume wake, bila shaka ni maneno mengi sana ya kuuchafua moyo wake.

Watu wa Mungu tunakutana na mambo mengi sana, mambo ambayo mengine yanakujia uso kwa uso yakilenga kukuondoa kwenye njia ya imani yako. Maana muda mwingine Mungu wetu huonekana hayupo nasi hasahasa tunapopita kwenye majaribu makali.

Haya hayataisha kamwe, cha msingi ni wewe kutengeneza uhusiano wako na Mungu ili unapokutana na maneno ya kukuvunja moyo kutokana na hali uliyonayo. Uwe na ujasiri wa kuendelea kusimamia imani yako, hata kama wanayosema ni kweli, uwe na nguvu ya kusema hawawezi kuwa na ukweli wa maisha yako kama aliyekuumba.

Rejea: Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika Kijulike kati ya mataifa machoni petu. ZAB. 79:10 SUV.

Hawataacha kusema pale wanapoona unateseka na kuumia, lazima watauliza yupo wapi Mungu wao wanaomwomba kila siku. Uwe tayari kupokea mashutumu hayo, maana yatakupata tu katika safari yako ya wokovu.

Utafika wakati machozi yako yatakuwa chakula chako, maadui zako watakucheka na kukupa maneno mabaya. Pamoja na hayo tumaini lako liwe kwa Bwana, misuli yako ya imani isimamishwe vyema na neno la Mungu.

Rejea: Ee BWANA, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako? Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu. Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao. ZAB. 80:4‭-‬6 SUV.

Pamoja na mambo hayo yote ya kuchekwa na kudharauliwa na wale wanaokuchukia wewe. Hakikisha moyo wako unaendelea kulitukuza jina la Yesu Kristo.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081.