Yeremia alikuwa nabii wa Mungu, nabii ambaye aliisema kweli ya Mungu siku zote bila kupindisha neno lolote la uongo.
Alikuwa ni nabii asiyeogopa kutoa unabii anaopewa na Mungu wake, haijalishi mazingira yalikuwa magumu kwake. Alihakikisha anatimiza wajibu wake kama nabii wa Mungu.
Alitokea mfalme ambaye alikuwa hapendi kweli ya Mungu, wala asiyesikia maneno ya Mungu. Mfalme huyo alikuwa anaitwa Sedekia.
Pamoja na mfalme Sedekia kutopenda maneno ya Mungu, alituma watu wake wakamwambie nabii Yeremia awawombee taifa lake kwa Mungu.
Rejea: Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa BWANA, Mungu wetu. YER. 37:3 SUV.
Huyu nabii Yeremia pamoja na kutokubaliwa maneno ya unabii wake anaopewa na Mungu, mfalme Sedekia alimtaka awaombee.
Unabii wa Yeremia ulionekana kama vile hutakii mema nchi aliyoongoza mfalme Sedekia, hilo likapelekea nabii Yeremia kukamatwa na kupelekwa gerezani.
Rejea: Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo. Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza. YER. 37:13, 15 SUV.
Nabii Yeremia hakukamatwa tu na kuwekwa gerezani, kwanza tunaona akisingiziwa kesi isiyo yake kwa kuambiwa anaenda kujiunga na Wakaldayo. Na pili alipigwa sana.
Tunajifunza nini hapa kupitia habari hii ya nabii Yeremia, nabii ambaye alikuwa anaisema kweli ya Mungu. Nabii ambaye pamoja na kusekwa gerezani, bado alikuwa anatoa unabii kwa wale wale waliomfunga gerezani.
Utumishi unaonekana unaanza kuwa mgumu pale unapokutana na uongozi wa nchi/mahali unapoishi, usiopenda ukweli kutoka kwa Mungu.
Na kazi kuu ya mtumishi wa Mungu ni kuisema kweli bila kukwepesha maana halisi ya ujumbe aliopewa na Mungu.
Shida inakuja pale unapousema ukweli ambao unaonekana una madhara kwa nchi, na madhara haya yanakuwa yameruhusiwa na Mungu mwenyewe yatokee.
Hapa tunajifunza kwamba, Mungu anakuwa amemruhusu mtumishi wake auseme ukweli huo, ili watu wale watakaposikia waweze kuacha matendo yao mabaya.
Cha kushangaza zaidi Mungu aliendelea kusema na nabii Yeremia akiwa gerezani, huko huko gerezani hakusita kutoa unabii wake pale alipoulizwa.
Hili linatupa ujasiri kwamba, Mungu wakati mwingine hawezi kupambana kukutoa katika gereza ulilofungwa. Humo humo ndani ya gereza ataendelea kukutumia kwa kazi yake.
Usiogope kutenda kazi ya Mungu, hata pale unapokutana na misukosuko ya kihuduma kama hii ya nabii Yeremia.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081