Tunakutana na changamoto mbalimbali katika maisha, pia katika utafutaji wa maisha tunapitia nyakati ngumu tofauti tofauti, zipo nyakati za kuumiza mioyo yetu, zipo nyakati za aibu, nyakati za kudharaulika kutokana na hali za maisha tunayoishi wakati huo.

Wapo vijana unaowaona wamefanikiwa leo ukirudisha picha ya miaka 10 au 20 nyuma unaweza kuwakataa leo, maana hawafanani kabisa na hali walizokuwa nazo kipindi hicho na sasa walivyo ni tofauti kabisa.

Zipo kazi ambazo vijana hupitia kuzifanya, kazi hizi kwa jamii huwa ni za aibu, mtu hayupo tayari kusema hiyo kazi kutokana na jamii inavyoichukulia, wakati mwingine hata wazazi wa binti wakisikia anaolewa na kijana mwenye kazi hiyo humkataza na kumwambia hapaswi kuolewa na mwanaume mwenye hiyo kazi.

Wapo pia mabinti wamejishusha thamani zao na kujiona wao ni wa kawaida sana, na kujiona kuolewa na mwanaume wanayemtaka haiwezekani kutokana na kiwango chao cha elimu au kazi wanazozifanya. Hii imewafanya kujidharau hata unapoongea naye unamwona amejikatia tamaa, kama sio kujikatia tamaa utamwona ni mtu wa kujikunyata.

Mazingira ya kiuchumi kwa vijana, kuzaliwa familia za kipato cha chini, kufanya kazi ambazo jamii zinaziona sio kazi za heshima, binti kuzaa mtoto akiwa nyumbani, kijana kukosa mahari muda mrefu, na mengine mengi yamewafanya wengi kujiona wao ni mapanzi.

Sasa kijana wa kiume anaweza kukutana na binti anayepitia baadhi ya nyakati ngumu akamwonea huruma, kumwonea huruma huko kukampelekea kumuoa. Kigezo anachotumia ni kumsaidia maisha aache kuteseka, lengo ni njema ila likitawaliwa na huruma tu bila upendo wa kweli hilo ni tatizo.

Mwanaume mwingine anaweza kumwonea huruma mwanamke aliyekaa umri mrefu bila kuolewa, akatokea kama yeye ni mkombozi, kama huruma hii haitakuwa na upendo wa kweli ndani yake uwe na uhakika ndoa hiyo itakuwa na shida.

Yafuatayo ni madhara 5 ya kuoa/kuolewa na mtu uliyemhurumia/uliyemwonea huruma;

  1. Kuchokana Mapema

Zile hamu zinazokuwepo wakati wa uchumba huwa ni nzuri sana, wakati mwingine usipokuwa makini unaweza usione kitu kibaya kwa mwenzako, wala unaweza usione udhaifu uliopo kwa mwenzako.

Watu wanapokujia na kukueleza kitu kinachotaka kuwatenganisha kinaweza kisipata nafasi kutokana na maisha mnayoishi wakati wa uchumba, wakati wa uchumba unaweza usimalize dakika 30 bila kuwasiliana na mwenzako.

Unapoingia kwenye ndoa mambo huwa sio hivyo, unaweza kujiuliza ni kwanini, tutaelezana siku nyingine, ila leo ninataka tuzungumzie madhara yake. Mtu aliyekuhurumia au uliyemhurumia anaweza kukuchoka haraka au unaweza kumchoka mapema, maana upendo wa kweli hukuwa ndani yako.

Kumhurumia mtu sio vibaya ila hakikisha unampenda kweli kutoka ndani ya moyo wako, na ni kusudi la Mungu kuishi naye, nje na hapo mtachokana kesho tu, na utaanza kujuta kwanini ulikubali kufunga ndoa naye. Maana sio kila wakati utakuwa unafarijiana naye na akiendelea kuendekeza ule udhaifu wake atakuchosha au utamchoka.

2. Kumnyanyasa/Kunyanyaswa

Yapo manyanyaso ndani ya ndoa yanayotokana na mwanaume/mwanamke aliyekuhurumia, anaweza kutumia udhaifu wako aliokukuta nao kukusimanga, mfano nisingekuwa mimi hadi sasa usingekuwa umeolewa/usingeoa, nilikuhurumia tu.

Kauli kama hizi zinaumiza sana, na zinaweza kugeuka manyanyaso kwako, sasa lazima uwe makini kuepuka manyanyaso haya yasiyo ya lazima, hupaswi kumhurumia mtu, kama unamhurumia msaidie tu ila sio kumuoa/kuolewa naye.

Manyanyaso mengine yanaweza kuwa mazingira aliyokukuta nayo kipindi hicho, kwa kuwa alikuhurumia na akajikuta amekuoa kama hakuwa mtu wako sahihi atakusumbua na atakuwa kero kwako. Tena zile kauli zake za kujirudia rudia kuhusu mazingira aliyokukuta nayo kabla ya kuoana zitakuwa zinakunyanyasa ndani ya nafsi yako.

3. Kutengana/Kuachana

Manyanyaso au masimango yakishazidi ni rahisi sana ndoa kuvunjika au kutengana, hili unaweza kuliepuka mapema kama kijana ambaye bado hujaingia kwenye ndoa. Huruma zisikutawale ukaacha kuangalia kusudi la Mungu, wala usijione wewe ndiye mkombozi kwa huyo mvulana au msichana.

Ikiwa kweli ni mke/mume wako hutasukumwa na maisha anayoishi, bali utasukumwa na upendo wa kweli juu yake, tunakutana na watu wengi tunaowahurumia kutokana na matatizo yao ila huwa hatuwachukui na kuishi nao.

Mara nyingi tunachokifanya kwao ni kuwasaidia kiasi cha fedha, au chakula, au kuwapa mitaji ya biashara, tunawaacha na kuendelea na maisha yao. Sasa kama utajidanganya ukaingia kwenye ndoa na mtu uliyemhurumia na sio kumpenda, uwe na uhakika mtatengana siku chache baada ya ndoa yenu.

4. Kutoneshwa kidonda

Ukihurumiwa au ukimhurumia msichana/mvulana ukamuoa/ukaolewa naye ujiandae na kukumbushwa yale maisha uliyoishi pale utakapomkosea, yale maisha ambayo hutamani kuyasikia maana yanakupa machozi kila ukikumbushwa.

Huruma kama tuliyoizungumza sana hapo juu na kama tulivyosema sio mbaya kama ikitumika sehemu sahihi, inaweza ikakuletea maumivu kwa kukumbushwa mambo ya zamani na huyo mwenzako aliyekuchukua au uliyemuoa kwa kumwonea huruma.

Hili la kuepuka kwa kijana ambaye unapata elimu hii, huruma ina kikomo, ila upendo wa kweli huna kikomo kwa mke/mume wako. Mnaweza kufurahia maisha ya ndoa hadi kifo kinawatenganisha, hata kama mtakutana na changamoto kwenye ndoa yenu bado upendo wenu utawalinda kwa kuendelea kuishi pamoja.

5. Wazazi Kuwachoka

Kwa kuwa hamkupendana bali mlikutanishwa na huruma, mnaweza kugeuka kero kwa wazazi/walezi wenu, mtakuwa na kesi zisizokuwa na kikomo, unaweza kuchukiwa na wazazi wa mke wako kutokana na mambo wanayosikia kwako.

Unaweza kuchukiwa na wazazi wa mume wako kutokana na maneno wanayoletewa na mtoto wao kuhusu wewe, wakati huo wanaweza wasijue chanzo cha hayo matatizo ni nini ila chanzo kinaweza kuwa msingi mbaya wa mahusiano yenu.

Kesi zisizo na kikomo ni kero kwa wazazi wako/wenu, wazazi wako wanaweza kukaa kimya na ukaanza kuwaona hawakupendi kumbe wamechoka na makesi yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Kwanini ufike huko hadi kuchokwa na wazazi kwa matatizo ya ndoa yako? Unao uwezo wa kufanya maamuzi sahihi sasa.

Mwisho, bila shaka umeshayajua madhara ya kuoa/kuolewa na mtu uliyemhurumia, mwana wa Mungu anayo huruma ndani yake ila sio huruma ya kuwaunganisha kwenye ndoa bila kumpenda. Umemhurumia mwenye njaa ya chakula mpe chakula, umemhurumia maskini msaidie hitaji lake, umemhurumia mgonjwa mpe pesa aende hospital, umemhurumia mwanamke aliyekaa miaka mingi bila kuolewa mwombee aolewe.

Hakikisha unayemuoa/unayeolewa naye umejithibitishia kutokana na hizi  Sifa Sita (6) Muhimu Za Kuweza Kumtambua Mke/Mume Wako Sahihi Wa Ndoa. – Chapeo Ya Wokovu (chapeotz.com) https://bit.ly/3oRQdP6 bonyeza hayo maandishi ya blue kujifunza zaidi.

Unapenda kufahamu jambo lolote kuhusu mahusiano, ama una changamoto yeyote kuhusu mahusiano, tuandikie ujumbe kwa email; samsonaron0@gmail.com au wasap na +255759808081. Changamoto yako inaweza kuwa somo kwa mtu mwingine ikamsaidia kutorudia kosa au ikamvusha sehemu aliyokwama.

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081