Mtu anaweza akawa mvumilivu sana, akavuka kila kikwazo katika maisha yake, sio kwa uwezo wake na akili zake. Kila kikwazo alichovuka, Mungu alimvusha na akabaki salama.

Akawa shuhuda mzuri hata kwa wale ambao hawajamjua Mungu, sio hilo tu, hata wale ambao bado hawajakomaa vizuri kiroho. Wanakuwa na mambo mazuri wanayojifunza kwa mtu huyo.

Lakini pamoja na uvumilivu wake wote, pamoja na kusifika kwake kwa uvumilivu wake, inafika mahali anaona haina haja ya kusubiri tena. Anaamua kuchukua maamzi ambayo sio mazuri mbele za Mungu.

Maamzi ambayo yana athari kubwa kwenye maisha yake ya kiroho na kimwili, wakati huo anafanya hivyo anakuwa anaona Mungu amechelewa kufanya au kutenda vile alimwomba.

Sio jambo geni kuona mtu ambaye alikuwa anasema ameokoka, mtu huyo kwenda kutafuta msaada kwa miungu mingine. Hadi anachukua hatua hiyo anakuwa ameona Yesu Kristo hana msaada kwake.

Sio ajabu kumwona kijana aliyekuwa mtu wa maombi sana, dada aliyesifika kwa bidii yake ya mambo ya Mungu. Baada ya kuona amesubiri sana kuolewa na hapati mwanaume wa kumwoa, akachukua maamzi ya kutembea na mwanaume bila utaratibu na kwenda kuishi naye.

Kungoja wakati wa Bwana ni muhimu sana, sio jambo jepesi kama tunavyoweza kutamka kwenye midomo yetu. Lakini kwa Mungu yote yanawezekana.

Haya ya kusubiri tunajifunza kutoka Biblia, tunaona Sauli akimsubiri Samwel, lakini hakufika kama ilivyotarajiwa afike.

Rejea: Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. 1 SAM. 13:8 SUV

Siku zote pale tunapochoka na kukata tamaa, ndipo mahali ambapo kile kilichotufanya tusubiri kwa muda mrefu, hutokea. Kinapotokea hukuta tayari mtu ameshafanya maamzi ambayo sio mazuri kabisa kwake.

Hili tunaliona kwa Sauli, baada ya kuchukua maamzi yake, ndipo yule waliyemsubiri kwa muda wa siku saba alifika. Ambaye alikuwa ni Samwel.

Rejea: Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. 1 SAM. 13:9‭-‬10 SUV.

Mara nyingi maamzi ambayo huwa tunachukua kwa kuchoka kwetu kusubiri, huwa sio maamzi sahihi. Yale ambayo ni sahihi huja na kukutana na jambo tofauti.

Madhara yake huwa makubwa, hubaki majuto, majuto ambayo hubaki kwetu, au kwa Mtu, pale anapojaribu kuweka sawa haitakuwa vile angesubiri wakati wa Bwana.

Samwel hakusita kumwambia moja kwa moja Sauli kile alifanya, hazikuwa taarifa njema sana ila ulikuwa ni ukweli. Kwa maana nyingine tunasema hayo ndio yalikuwa matokeo ya uamzi aliouchukua pale alipochoka kusubiri.

Rejea: Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. 1 SAM. 13:13 SUV.

Hatupaswi kufanya haraka, hasa pale tunapokuwa tumepeleka mahitaji yetu mbele za Mungu. Kujichukulia maamzi yetu mikononi pasipo kufuata utaratibu wa kiMungu, maamzi yetu yatageuza majuto yasiyo na kikomo katika maisha yetu.

Kosa alilolifanya Sauli, lilimfanya akataliwe moja kwa moja na Mungu, hapo hapo Mungu akawa amejichagulia mfalme wake mwingine anayemfaa.

Rejea: Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru. 1 SAM. 13:14 SUV.

Yapo mambo ukishaharibu umeharibu, hayana/hayakupi nafasi ya pili, hapa Sauli hakupewa nafasi ya pili. Kwa sababu ya kutotii maagizo ya Bwana aliyopewa, kwa maana nyingine alikuwa anajua sadaka huwa inatolewa na kuhani. Na yeye hakuwa kuhani.

Mungu wetu hawahi, wala hachelewi, tunapaswa kusubiri wakati wa Bwana. Tukichoka kusubiri na kuamua kufuata njia zetu, tuwe na uhakika madhara yake ni makubwa kuliko tungesubiri.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81