Bwana Yesu asifiwe, leo tunaenda kujifunza somo hili muhimu sana, kama upo bize sana au unaona hili somo ni masomo kama masomo mengine uliyoyazoea unaweza kuendelea na shughuli zingine kwanza. Alafu baadaye ukiwa tayari utarudi kusoma au kujifunza, kama huo muda utakuwa nao, japo sio rahisi kurudi au kukumbuka. Nikuambie kwamba hili somo linaweza kubadilisha maisha yako ukizingatia utakayojifunza.
Siku hizi sio jambo la ajabu sana kumkuta kijana wa kiume na kike wakiwa katika mahusiano ya mapenzi, huku wakiitana mke na mume, limekuwa jambo la kawaida kabisa. Hata kama wazazi bado hawajapokea taarifa yeyote unakuta haya mambo yanafanyika kwao.
Leo tutazungumza hasa madhara ya kufanya mapenzi kabla ya ndoa, baada ya somo hili ninaamini Roho Mtakatifu atakuwa ameongea na wewe kwenye eneo fulani kama kijana ambaye bado hujaoa/hujaolewa. Na kama tayari upo kwenye ndoa kuna kitu utajifunza pia.
Kabla ya kwenda mbele sana naomba usome kisa hichi cha kweli ndani ya Biblia, soma kwa umakini na kwa kurudia. Ukisoma vizuri na kukielewa utaweza kunielewa vizuri zaidi wakati tunaendelea kujifunza somo letu hili;
“Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. 2 Sam 13:10-15 SUV.”
Sio ajabu wakati unasoma ujumbe huu umeachwa na mtu uliyekuwa na asilimia nyingi za kumuoa/kuolewa naye, huenda sio mmoja, umeachwa au umeacha wasichana/wavulana zaidi ya wawili au watatu au zaidi.
Nataka sasa ujue sababu za kuachwa huko, zipo nyingi ila leo tutazungumza eneo la kukutana kimwili, maana wengi huwa hatuelewi kwanini tunaachwa au tunaacha. Huenda umekaa umekata tamaa ya kuoa/kuolewa kwa kuumizwa kila wakati kwa kuachwa.
Tukirudi kwenye kisa chetu hapo juu tunaona vijana wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume, ambao ni Amnoni na Tamari. Ukisoma kisa hichi sura nzima ya 2 SAM. 13 utaona shida ilianzia kwa Amnoni ambaye ni mwanaume, ikaenda hadi wakazini na Tamari.
Ninachotaka ukione hapo ni nini? mara nyingi sana vijana huwa tunaendeshwa na tamaa za mwili, kijana wa kiume anampenda binti fulani si kwa sababu nyingine. Anakuwa anasukumwa na tamaa za mwili, ule upendo kabisa wa kuishi naye kama mke na mume unakuwa haupo.
Ukitaka kuthibitisha hili, siku wakikutana kimwili utaona ule msukumo wa upendo uliokuwepo kati yao unapungua au unatoweka kabisa. Vile kijana wa kike alikuwa anamwona kijana wa kiume, ule mtazamo unabadilika kabisa, kule kuheshimiana kunaondoka kabisa.
Tunaona Amnoni alikuwa anampenda sana Tamari hadi akaugua ugonjwa ambao ulimfanya akonde siku hadi siku, siku wanalala naye au siku anafanya naye uasherati. Baada tu ya kumaliza alichokitaka kwa Tamari alimchukia na kumfukuza atoke ndani kwake, sijui kama unanielewa? Hebu jiulize mtu aliyempenda anamchukiaje baada ya kulala naye?
Uone shetani alivyomjinga, anawadanganya watu kuwa kusubiri hadi ndoa ndipo ufanye tendo la ndoa ni mambo ya kizamani, lakini wanaomsikiliza wameachiwa makovu mengi kwenye mioyo yao.
Kijana anaweza akajiona ana mkosi kwa kuachwa au kuacha kila mara, kumbe shida ipo hapa kwenye kuanza kufanya tendo la ndoa(uasherati) kabla ya ndoa. Tena maumivu yake huwa makali sana kupita yule ambaye alikuwa hajafanya hilo tendo, yaani kuachwa na mtu ambaye hamjalala naye haina maumivu kama yule mliyelala naye.
Wapo wengine wameachwa kwa sababu ya misimamo yao ya kukataa kufanya uasherati, wakati mwingine wanajiona wajinga kwa kusimama na huo msimamo wao. Hapana msimamo wao upo sahihi isipokuwa wale wanaokuja kwao na kuwataka wafanye hivyo ni tamaa tu zinawasukuma, wanapaswa kujiangalia maisha yao na uhusiano wao na Mungu ukoje.
Inawezakana makundi waliyonayo yanawafanya wawavutie wenye tamaa mbaya, au maisha yao wanayoishi yanawashawishi wanaume/wanawake kufanya nao uasherati, au mavazi yao yanawafanya waonekana ni watu wa kuchezea tu.
Dada yangu, kaka yangu, mdogo wangu, ukitaka kubaki salama na upunguze visa vya kuachwa kwa aibu, acha tabia ya kulala na wanaume/wanawake kabla ya ndoa. Hii ni hatari kimwili na kiroho, unaweza kuona ni ujanja ila ni jambo ambalo linaharibu maisha yako.
Nimejaribu kukueleza madhara yanayotokea baada ya kulala na kaka/dada, hasa kwa wadada inawaumiza kwa sababu wanaweza kuachiwa mimba. Wakaka hawapati ujauzito, nikiwa na maana madhara yao hayaonekani haraka, wadada wanaathirika moja kwa moja, na wakati mwingine wasimwone baba wa mtoto kwa miaka mingi baada ya kupewa ujauzito.
Tuwe makini, ukiacha jambo hili kuwa ni dhambi mbele za Mungu, jua ya kwamba linakuathiri moja kwa moja, achana na tabia ya kulala hovyo na wanaume/wanawake. Utaendelea kumtafuta mchawi wa maisha yako, kumbe ni wewe mwenyewe umeruhusu hayo yakutokee.
Unayemwona anakupenda mwambie avumilie hadi ndoa, kama ni dada usijifanye unajua sana kupika ukaenda kwa mwanaume kumpikia, yatakukuta ya Tamari, kama umesahau yaliyomkuta rejea kusoma tena hayo maandiko hapo juu.
Kijana wa kiume ili uache kuwakinai wadada hasa wale ambao mnataka kuingia kwenye ndoa ila ghafla unashangaa humpendi, achana na tabia ya kulala nao au kufanya nao mapenzi. Hii inasababisha kuwaona hawafai, hii haijaanza kukutokea wewe imeanza kwa AMNONI tuliyemsoma hapo juu, acha kutanguliza ngono mbele utakuwa usalama wako.
Labda unajiuliza utawezaje kuacha ngono, YESU yupo anaweza kukusaidia, mpe YESU maisha yako, utasema mbona nipo kanisani muda mrefu ila nimeshindwa kuacha. Kuwa kanisani sio kuokoka, unaweza ukawa kanisani na ukawa mpangani tu kama yule aliye nje ya kanisa. Amua kutoka moyoni mwako kuachana na tabia mbaya, alafu tubu kwa kumaanisha, kisha mruhusu Roho Mtakatifu awe kiongozi wa maisha yako.
Mwisho, maisha ya ujana bila ngono yanawezekana, ni wewe kuchukia hiyo hali na kumruhusu Mungu akuongoze katika maisha yako, na siku ukiamua kuoa/kuolewa itakuwa rahisi maana uhusiano wako na Mungu utakuwa vizuri. Tena hutapata changamoto kujua chaguo lako sahihi ni lipi.
Mungu akubariki sana
Ndugu yako katika Kristo
Samson Ernest
0759 80 80 81