Katika maisha haya, Mungu anaweza kumfanikisha mtu mali nyingi, anaweza akawa na mashamba ya kutosha, anaweza akawa na nyumba za kutosha, anaweza akawa na fedha nyingi, na vingine vingi vinavyofanana na hivyo.

Mtu mwingine anaweza akawa na nafasi kubwa kwenye jamii yake inayomzunguka, anaweza akawa ni kiongozi kwenye nafasi fulani nyeti serikalini. Ambayo hiyo nafasi kila mmoja anatamani awe yeye ndiye mwenye hiyo nafasi.

Mtu mwingine anaweza akawa ni mtumishi wa Mungu katika eneo la kiroho, katika nafasi yake akawa na nguvu kubwa ya kumzalia Bwana matunda mema. Akatokea mtu mwingine ambaye hayupo kwenye hiyo nafasi, akatamani yeye ndio awe kwenye hiyo nafasi ya huyo mtumishi wa Mungu.

Katika kutamani huko akaanzisha mpango wa hila kumwong’oa mwenzake kwenye nafasi hiyo, mpango ambao una nia ya kumpoteza kabisa huyo mtumishi wa Mungu, au kiongozi wa serikali.

Mipango hiyo mibaya inaweza kufanikiwa na kumwangamiza kabisa huyo mtumishi wa Mungu, au kiongozi wa serikali. Anaweza kuawawa, anaweza kufukuzwa kazi, anaweza kushushwa cheo kwa kuchafuliwa sifa yake ili aonekane hafai.

Lengo lao hiyo nafasi yake aipoteze na mwingine aichukue, mwenye kuitaka hiyo nafasi anaweza akawa ndiye aliyehusika kumwangamiza, au anaweza asiwe yeye akawa mtu mwingine wa karibu yake.

Haya sio mimi Samson nimeyatunga, bali ni mambo ambayo yapo ndani ya biblia yako. Yupo mtu aliyetamani shamba la mwenzake, baada ya kumwendea mhusika, huyo mhusika alikataa kuligawa shamba lake.

Mwenye shamba alivyokataa, yule aliyekuwa analitaka aliumia sana, alivyofika nyumbani kwake. Mke wake alimhoji, maana alikuwa ni mwanaume, alivyomweleza mke wake kinachomsibu, mke wake alimwahidi atalipata hilo shamba.

Hebu tuende pamoja, tujifunze kwa kupitia maandiko ya Biblia, tuwafahamu hao watu kwa majina kabisa. Uone vile ubaya unavyoweza kutengenezwa kwa mtu asiye na hatia, na ubaya ule ule ukamrudia aliyeutengeneza.

Rejea: Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. 1 FAL. 21:2 SUV.

Ahabu alitaka apewe shamba na Nabothi kama tulivyosoma katika mstari huo, Ahabu alimweleza moja kwa moja Nabothi sababu za kulitaka hilo shamba.

Unajua unapoomba kitu kuna kukubaliwa, na kuna kukataliwa, uwe unataka kununua kwa pesa zako nyingi. Ama uwe unaomba upewe bure, sasa Ahabu ombi lake halikukubaliwa na Nabothi.

Rejea: Nabothi akamwambia Ahabu, BWANA apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. 1 FAL. 21:3 SUV.

Baada ya Ahabu kupewa hayo majibu, yaani baada kukataliwa, ilimuuma sana. Tunaweza kusema hakutegemea kunyimwa, kwa asilimia fulani alikuwa na uhakika atapewa.

Tunaona kupitia haya maandiko hapa chini ninayoenda kukushirikisha, akiwa amekasirika, sababu hasa ya kukasirika kwake ni ile ile ya kunyimwa shamba.

Rejea: Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. 1 FAL. 21:4 SUV.

Kitendo cha kufikia kujilaza kitandani na kukataa kula chakula, kilimpelekea mke wake Yezebeli kumhoji. Yezebeli ni yule aliyemfanya Elia kukimbia na akafika mahali akaomba kufa, unaweza kurejea 1 FAL. 19 utakutana na habari kamili ya Elia.

Hebu turejee maandiko tuone vile mke wake Ahabu alimuuliza;

Rejea: Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? 1 FAL. 21:5 SUV.

Tunapata kujifunza jambo hapa, wakati mwingine mwanaume akivurugwa na mambo huko nje, na moyo wake ukawa na huzuni anaweza asile chakula.

Kama mwanamke hatamwelewa mume wake anaweza akaanza kuongea maneno yasiyofaa, tena yale ambayo yapo nje kabisa ya lengo. Lakini kwa Yezebeli ilikuwa tofauti, baada ya kuelezwa sababu, ona vile alivyomwambia mume wake Ahabu.

Rejea: Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. 1 FAL. 21:7 SUV.

Unaona hiyo kauli au majibu ya Yezebeli? Akamwambia mume wake hivi;
Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.

Akambembeleza mume wake kwa maneno hayo, sio kana kwamba aliongea kwa kubahatisha, aliongea kwa kumaanisha kweli atampa hilo shamba alilolinyimwa.

Atampaje sasa? Swali zuri, majibu yake ndio kiini cha somo hili, utaona vile ambavyo hila ilitumika kulichukua shamba la Nabothi.

Rejea: Mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. 1 FAL. 21:10 SUV.

Sijui kama umeelewa huo mstari, unaweza ukarudi kuusoma tena, hayo ni mazungumzo ya Yezebeli, anawaagiza watu wake juu ya Nabothi.

Wanapewa jukumu la kwenda kutengeneza kesi, ili wapate uhalali wa kumuua Nabothi, kumbuka kinachotafutwa hapo ni shamba.

Wale watu waliotumwa na Yezebeli na wao walikuwa waaminifu, walienda kufanya vile waliagizwa na Yezebeli wafanye.

Rejea: Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. 1 FAL. 21:13 SUV.

Hadi hapo kilichomwondoa Nabothi duniani ni shamba lake, shamba ambalo lilikuwa mali yake, hakumnyang’anya mtu yeyote, halikuwa shamba la magendo. Bali lilikuwa ni shamba alilorithishwa.

Pamoja na lilikuwa shamba lake, watu wabaya walimzulumu uhai wake, familia ikakosa au ikapoteza mtu wao muhimu kwa hila mbaya za watu wabaya.

Baada ya zoezi lao kukamilika, Yezebeli alimweleza mume wake Ahabu kuwa Nabothi amekufa, maana yake hakuna tena kizuizi.

Rejea: Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki. 1 FAL. 21:16 SUV.

Unaona hapo, Ahabu hakuchelewa, alianza safari ya kwenda shambani, ili alimiliki hilo shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.

Wakati anafurahia hilo la kwenda kumiliki shamba, huku upande mwingine mambo yalikuwa tofauti. Laiti angejua mpango wake mbaya umemchukiza Mungu, asingefurahia kwenda kulichukua shamba.

Rejea: Neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. 1 FAL. 21:17‭-‬18 SUV.

Sijui kama kuna jambo unajifunza hapo, mipango mibaya inaweza kufanikiwa kwa sehemu ila uwe na uhakika Mungu ataingilia kati.

Kumuua Nabothi haikuwa sababu sana, kumpoteza mtu fulani uhai wake, au kumwondoa mwenzako kwenye nafasi aliyokuwa nayo kwa kumtengenezea baya. Sio uhakika wa wewe kuimiliki hiyo nafasi yake.

Wakati Ahabu akifikiri mambo mengi juu ya shamba, wakati Yezebeli anafikiri amefanikiwa kumwondoa Nabothi uhai wake. Ujumbe wa Mungu ulikuwa njiani kwenda kwa Ahabu.

Rejea: Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. 1 FAL. 21:19 SUV.

Hili ni funzo kwetu, tusifanye mambo mabaya, tusitafute cheo kwa kuwapoteza wengine kama ilivyotokea kwa Nabothi kuzulumiwa uhai wake.

Tusitafute mali kwa kuwaua wengine ili sisi tumiliki, kufanya hivyo tunajitafutia laana mbele za Mungu. Tena tuwe na uhakika hatutayafaidi yale tuliyoyapata kwa hila.

Tumwombe Mungu atupe yeye yale tunayoyataka yawe yetu, tusipite njia zisizo sahihi kupata yale tunayotaka sisi. Madhara yake ni makubwa kama tulivyojifunza katika somo hili, epuka sana hili.

Mwisho, nakukumbusha umhimu wa kusoma neno la Mungu kila siku, hili ni jambo la muhimu sana katika maisha yako ya wokovu. Usiache kufanya hivyo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
+255759808081.