Asifiwe Yesu, ninayo sababu ya kumshukuru Mungu kwa uzima anaoendelea kunipa, amenipa kibali kingine tena cha kuweza kushirikishana maneno yake mazuri ya kututia nguvu ya kusonga mbele.
Huwezi kuelewa sana kama hujawahi kupita kwenye changamoto kiasi kwamba kila unayejaribu kumshirikisha jambo lako, anaona hawezi kukusaidia kulibeba. Sio kwamba hawataki, wanapima jambo lenyewe wanaona kabisa ni zito kwao kulibeba.
Huenda huwezi kuelewa vizuri sana kama hujawahi kupita katika kipindi ambacho watu wanakuwa pamoja na wewe siku za mwanzo, ila baadaye wanaona hawawezi tena kuendelea kukusaidia. Hapo ndio unakuwa mwisho wa mwanadamu kukusaidia jambo lako.
Kuna mwaka nilikuwa napita kwenye kipindi kigumu sana, nilikuwa sina pesa mfukoni na nilikuwa sina shughuli ya kueleweka kunifanya niingize pesa. Sasa ilikuwa ikifika muda wa kula nikiwa kwenye mizunguko ya hapa na pale, najisikia mzito kwenda nyumbani si unajua kuna ka aibu wenzako wote wanakuwa hawapo huo muda nyumbani, na kuendelea kukaa pesa ya kuingia mgahawani kupata chakula sina.
Siku moja kuna ndugu mmoja nikamwomba anitoe lunch siku hiyo, alivyofanya siku ya kwanza, siku ya pili ilipidi apite njia nyingine kunikwepa. Sio kwamba alikuwa anakosea kufanya hivyo, huo ndio ulikuwa mwisho wake wa kutoa msaada kwangu, hata kama alijua sina kazi inayoniingizia pesa alistahili kufanya hivyo. Maana na yeye ana bajeti zake.
Nilitembea na hali ile, ikiwa inanitesa sana kichwa changu, namshukuru Mungu alikuwa ananifundisha maisha kupitia hali ile. Na ilinifanya nitoke kwenye usingizi mzito sana niliokuwa nao kipindi hicho.
Zipo nyakati kama hizi, nyakati ambazo hata wale marafiki zako wa Karibu wataogopa kuambatana na wewe. Maana wanajua wewe ni mzigo, huwezi kujitegemea mwenyewe mpaka watoe pesa zao mfukoni. Na wanajua wana bajeti zao, ambazo wanapaswa kuzitekeleza ili wafikie malengo yao.
Nyakati hizi zinaambatana sana na kipindi upo nyumbani kwenu unategemea chakula cha familia ule. Kazi huna wala jeuri ya kujinunulia chai na chakula cha mchana huna, hata mdogo wako akikuomba pesa ya penseli unamwambia huna, na huna kweli.
Inafika kipindi anakuona huna jipya na wakati mwingine anaweza asikusalimie, unaweza kuanza kuziomba salamu na kuanza kutoa adhabu kwa wadogo zako kwa sababu tu wameonyesha dharau.
Inafika kipindi unaumwa kiasi kwamba watu wanakukatia tamaa na kuanza kuongea maneno yao wanayoona wao yanafaa kwao. Unaweza kutamani ukae na watu karibu ila wakawa hawapendi ukae nao Karibu, kwa sababu unatoa harufu mbaya ya ugonjwa wako.
Hichi kipindi ndicho kilichomkuta mtumishi wa Mungu Ayubu, ilifika kipindi hata watoto wadogo wanamradharau kwa jinsi alivyokuwa apigwe na ugonjwa.
Rejea; Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. AYU. 19:18-20 SUV.
Unapofika kipindi kama hichi cha kuchekwa na kudharauliwa na kuachwa na marafiki zako, ni wakati ambao utapaswa kusimama na Mungu wako. Hapa ndipo ile akiba ya uhusiano wako mbele za Mungu uliyokuwa nayo wakati huna shida, itaanza kutumika.
Wakuambatana naye kwa ukaribu sana ni Mungu wako, nakwambia wanadamu wanaweza kukugeuka usiamini kama walikuwa ni watu wako wa karibu. Tumejionea hili mara nyingi kwa macho yetu, haihitaji kuumiza sana kichwa kuanza kutafuta ukweli wa hili jambo.
Jiandae na jiwekee mikakati ya kuwa na uhusiano mzuri zaidi wa kuwa karibu na Mungu kuliko kitu chochote. Penyeza kila njia kuhakikisha unaulisha moyo wako Neno la Mungu, hakikisha hukosi ibada za kanisani, hakikisha unawatendea wengine mema kwa kadri ya nafasi yako.
Mungu hatakuacha kamwe wakati wa shida yako, atakuinulia mambo yako utabaki unamshangaa.
Mungu akusaidie uweze kuelewa zaidi hili jambo kwa upana wake.
Fb; Chapeo Ya Wokovu.
E-mail; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.