Leo tunatimiza mwaka mmoja tangu tufunge ndoa na mke wangu Rebecca ambayo ilikuwa tar 21/10/2017 siku tuliyofunga ndoa, yapo mambo machache ninatamani kuyazungumza hapa hasa yaliyoujaza moyo wangu kwa furaha.

Utasema ili iweje, mwaka mmoja tu unaona kitu cha ajabu sana wakati wengine tupo mwaka wa 5 au 10 sasa lakini hatusemi kitu. Na kweli mwaka mmoja sio kitu cha ajabu sana ila ndani ya mwaka mmoja yapo mambo niliyoyaona na kujifunza baada ya kuoa, na sikuyaona kabla ya kuoa.

Watalaamu wanasema ili mfahamiana vizuri na mke/mume wako ni mpaka mfikishe miaka 5 ila nashangaa kwenye biblia yangu haipo kabisa hicho kipimo cha hiyo miaka.

Ndio haipo kibiblia ila watu walikaa tu wakaona hilo, pamoja na kuona hilo, unaweza kukaa kwenye ndoa zaidi ya hiyo miaka mitano na ndoa yako ikaharibika vile vile, kama hutoishi kama Neno la Mungu linavyoelekeza.

Rejea: Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe. Waefeso 5:33.

Hapo inaposema “kila mtu ampende mke wake” ni sawa na kusema kila mwanaume na amepende mke wake, maana yake mtu ni mwanaume kwenye huo mstari.

Kwa hiyo ndoa ina kanuni zake kibiblia na ukizivunja hizo kanuni, ukaanza kwenda unavyotaka wewe, haijalishi upo kwenye ndoa mwaka wa kumi sasa. Uwe na uhakika hiyo ndoa itasambaratika kabisa na itabaki historia, wala haijalishi mna watoto wangapi kwenye ndoa yenu.

Ndio kuna kanuni ambazo Mungu mwenyewe ameziweka wazi kupitia Neno lake, nimekushirikisha mstari hapo juu kutoa kitabu cha Efeso 5:33. Tena maandiko matakatifu yanaendelea kusema hivi;

Rejea: Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. EFE. 5:22‭, ‬25 SUV.

Haleluya, Mke anapaswa KUMTII mume wake, na Mume anapaswa KUMPENDA mke wake, kumbe mke anahimizwa kumtii mume wake. Inaonyesha wazi hitaji la mume kwa mke wake ni kuona mke wake anamtii.

Pia inaonekana hitaji kubwa kwa mke ni kuona mume wake akimpenda, sio upendo wa mdomoni tu ni ule upendo wa ndani kabisa. Maana ukimpenda mke wako hutoweza kumfanya kitu kibaya, tena upendo wenyewe unaozungumzwa hapa ni ule upendo wa Kristo aliyejitoa kwa ajili ya maisha yetu.

Usipofanya hayo uwe na uhakika ndoa yako haitakuwa salama, haijalishi una umri gani kwenye ndoa yako. Hata kama utasema nini, Neno la Mungu ni amina na kweli.

Kabla ya kuoa nilikuwa nakutana na maneno mengi sana kuhusu ndoa, tena nikitaka kumshauri mtu aliye na mtazamo hasi juu ya wanaume/wanawake kutokana na vile ametendewa kitu kibaya. Wengi walikuwa wanakimbilia kusema ukioa utaona, hawajui kuwa mimi nilikuwa nasoma biblia.

Matisho hayo yote hajawahi kunibadilisha mtazamo wangu juu ya Neno la Mungu, nilichokuwa najua ni kwamba ndoa ni nzuri sana. Haijalishi changamoto nilizokutana nazo Kabla sijaoa, haijalishi niliwahi kuumizwa na mahusiano ya kuelekea kwenye ndoa.

Baada ya kuoa sasa nimeona mambo mengi sana yamebadilika, yapo mengi sana ila kikubwa ninachoona nina utulivu mkubwa sana kuliko huko nyuma kabla sijaoa. Yale Matisho ya watu wenye mtazamo hasi juu ya wanawake kwangu imekuwa tofauti kabisa.

Tena nikathibitisha hili andiko lifuatalo kwa vitendo kuwa ni kweli na kwangu nimeliona kabisa likifanya kazi, hebu tusome hili andiko;

Rejea: Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana. Mithali 18:22.

Kweli kabisa baada ya kuoa nimeona kibali cha Bwana kikiwa juu yangu tofauti kabisa na kabla sijaoa, sio kwamba nilikuwa sijaokoka la hasha.

Kwa mwaka huu mmoja nimeona uzuri wa kuoa tofauti kabisa na ubaya niliokuwa naelezwa huko nyuma. Na ninaoendelea kusikia watu wakiuzungumza siku zote.

Naendelea kumtukuza Yesu Kristo kwa hili, aendelee kututunza na mke wangu Rebecca siku zote za maisha yetu hapa duniani.

Neno la Mungu linasema hivi; Mwanamke mwema ni taji ya mumewe… Mithali 12:4(a) nami naiona taji nzuri aliyonipa Mungu, taji yenyewe ni Rebecca(mama Avisha)

Sina budi kumrudishia Mungu Sifa na utukufu kwa kunipa mke mwema, naamini alijua ataweza kusaidia kusudi aliloweka ndani yangu.

Mungu akubariki sana wewe unayeendelea kutuombea.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.