Yawe maneno mazuri sana anayozungumza mtu, ama yawe ni maneno mabaya sana anayozungumza mtu. Hiyo ni hazina iliyo ndani ya moyo wake, haneni kwa bahati mbaya, ananena yaliyoujaza moyo wake.

Mtu anaweza kujitetea kwa maneno aliyotamka, kuwa ametamka kwa bahati mbaya, kuwa ulimi ulitereza, anaweza kujitetea kwa vyovyote vile ila ukweli ni kwamba hicho ndicho kimeujaza moyo wake.

Hakuna bahati mbaya ya kutokwa na maneno machafu, mtu anatokwa na kitu ambacho kipo ndani ya moyo wake. Kujitetea atajitetea sawa, kuwa halikuwa kusudi lake kunena maneno ya namna hiyo ila fahamu hazina yake ilikuwa imehifadhi hayo maneno.

Ni rahisi sana kumtambua mtu aliyeokoka muda sio mrefu, wakati akiwa anafanya mambo mabaya ya Duniani, hayo mambo ilikuwa ni hazina iliyo ndani ya moyo wake. Anapookoka, kuna masalia yatakuwa ndani yake ila kadri anavyozidi kukua kiroho hayo masalia yanatoweka kabisa.

Kwahiyo unapokutana na mtu akakutamkia Neno la hovyo, usianze kushindana naye sana, wewe fahamu ametamka yaliyoujaza moyo wake. Ukitaka kumsaidia, uwe unajua pa kuanzia, usianze kushindana naye kwa nje tu, utakwama.

Hatokei tu mtu akawa ananena maneno mazuri, maneno yenye kujenga, maneno ya hekima, maneno yenye kumtoa mtu hatua moja kwenda nyingine. Anachokuwa nacho huyu mtu ni ile hazina iliyoujaza moyo wake, ndiyo inamfanya huyo mtu anene hayo ayanenayo.

Mzazi kumtakia mwanaye maneno ya hovyo kama vile; mbwa wewe, ng’ombe wewe, sura mbaya kama ya baba yako, haya maneno huwa hayatoki hewani, ni vitu vilivyoujaza moyo wake. Hazina hii ya maneno mabaya ni kubwa ndani ya huyu mzazi, hapo anatimiza tu andiko.

Rejea: Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. LK. 6:45 SUV.

Haitatokea mti mbaya ukazaa matunda mazuri, wala haitatokea mti mzuri ukazaa matunda mabaya, muembe utazaa maembe, mpapai utazaa mapapai, mkorosho utazaa korosho, mchungwa utazaa machungwa.

Rejea: Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. LK. 6:43‭-‬44 SUV.

Ndivyo ilivyo kwa mtu, moyo wa mtu ukiwa una hazina ya maneno mabaya, kinywa chake kitatamka maneno mabaya. Vilevile moyo wa mtu ukiwa umejaa hazina ya maneno mazuri, kinywa chake kitatamka maneno mazuri.

Umewahi kusikia mtu anasema, ngoja nikanywe pombe fulani atanikoma, au umewahi kuona mtu amelewa alafu anawatukana watu maneno mabaya, au umewahi kutukanwa mwenyewe na mtu wako wa karibu. Alafu watu wanasema hiyo ni pombe tu, hapana, hiyo sio pombe tu, ni hazina iliyo ndani ya moyo wake.

Maneno mabaya yanayomtoka mlevi yeyote sio kwamba yametengenezwa na pombe aliyoinywa, matusi anayotukana yalishakuwepo kabla hata ya kunywa pombe. Pombe imetifua kisima cha maneno yaliyoujaza moyo wake.

Asikudanganye mtu ilikuwa bahati mbaya kukutamkia maneno mabaya, hiyo ni hazina iliyo ndani ya moyo wake. Maneno mabaya au mazuri huwa hayatoki hewani, utasema wapo huongea maneno mazuri ila ni watu wabaya sana.

Huo ni utapeli wa muda mfupi tu, kama umewahi kupigiwa simu na wale matapeli wa mitandao (kama ni wakala wa Tigopesa, M-pesa, Airtel money utakuwa unaelewa vizuri) hawa matapeli ukishawagundua huwa wanatoa matusi mabaya sana. Unaona alikuwa anakuongelesha kwa maneno mazuri, ghafla matusi yanayomtoka wapi? Unaweza kuona hazina iliyo ndani ya moyo wa mtu ilivyo ngumu kuificha muda wote.

Umeokoka na bado kinywa chako kinatoka maneno mabaya, unapaswa kutoka humo haraka, jaza moyo wako maneno mazuri, maneno mazuri yanatoka kwa Bwana. Soma sana Neno la Mungu, jiondoe kwenye makundi mabaya, soma vitabu mbalimbali vyenye mafundisho mazuri ya kujenga, acha kusoma vitabu vyenye maadili mabaya, acha kusoma jumbe/makala ambazo zinatengeneza hazina ya maneno mabaya ndani yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081