Haleluya,
Tunaposema kwa fulani kuna Matanga, usije ukafikiri ni mmea fulani unaoitwa matanga.
Matanga ni maombolezo yanayotokana na msiba wowote ule, unaweza kuwa msiba wa kumpoteza ndugu yako, mtoto wako, mzazi wako, mke wako, mume wako na rafiki yako au jirani yako wa karibu.
Hayo ndio yanaitwa matanga, kwa lugha nyingine tunaweza kusema ni maombolezo.
Naendelea kuipenda biblia siku hadi siku kadri ninavyozidi kuisoma, naona kufunguliwa na kumwelewa Mungu alivyo mzuri kwetu kupitia Neno lake.
Ukiachana na kufiwa, yapo matanga ya watu kwenye ndoa zao, kuna wanandoa wanaomboleza usiku na mchana juu ya waume zao au wake zao.
Kuna watu wana matanga juu ya biashara zao, wanaomboleza usiku na mchana kwa jinsi vile wameingia hasara.
Kuna watu wana matanga kwa kutafuta kazi ya kuajiriwa, wamefanya hivyo muda mrefu na bado hawajapata.
Pamoja na hayo yote, Yesu Kristo anasema ukiwa kwake, hiyo mizigo yote ataitua. Haijalishi unaona giza mbele yako, kama mahusiano yako na Mungu yapo sawa uwe na uhakika Bwana hatakutupa kamwe.
Rejea: Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha. ZAB. 30:11 SUV.
Kama Mungu anaweza kukuvua vazi la huzuni na akakuvika vazi la furaha, kwanini using’ang’ane na yeye ili akuondolee tabu hizo zote.
Hujawahi kuona mtu anapitia wakati fulani hivi mgumu lakini ghafla mnamwona anazidi kustawi na kusonga mbele. Unaweza kufikiri anajifanyisha kumbe ndivyo ilivyo.
Walio ndani ya Kristo wana ujasiri mkubwa mno, usifikiri ni hasara kuokoka, usikifikiri ni majuto kukaa na Yesu Kristo moyoni mwako.
Neno la Mungu linasema; BWANA atawapa watu wake nguvu; BWANA atawabariki watu wake kwa amani. ZAB. 29:11 SUV.
Kupitia andiko hili, unaweza kumdai Mungu haki zako. Kama unaona kuna matanga unapitia nayo, ameahidi kukutia nguvu na kukupa amani ya moyo wako. Tena atakuvua gunia la maumivu yako na kukuvika furaha ya kudumu.
Unajua mwenyewe una matanga gani katika maisha yako, NENO linasema utavuliwa gunia la Maombolezo na kuvikwa vazi la furaha ndani ya maisa yako.
Utashangaa katikati ya majaribu yako unamtukuza Yesu Kristo kwa viwango vya juu zaidi. Kwa sababu ndani mwako una tambua uweza wa Mungu aliokutendea katika maisha yako.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.