Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, hongera kwa kuchaguliwa tena siku ya leo ukiwa bado u uzima. Haijalishi changamoto ulizokutana nazo, bado Mungu ni mwema kwako anaendelea kukupigania.

Utoaji sadaka umechangia asilimia kubwa sana waamini wengi kushindwa kuelewa upi ni utoaji sahihi mbele za Mungu, na upi si utoaji sahihi mbele za MUNGU. Kutokana na mafundisho mbalimbali ambayo yanatolewa sana, mengine akiwa yanatisha ili utoe na mingine hayatishi ila yamekuacha tu njia panda.

Ukweli usiopingika ni kwamba yapo mafundisho potofu sana, ambayo nia yake si wewe utoe kwa ajili ya kazi maalum ambayo inaenda kufanyika kwa ajili ya Mungu. Bali ni tamaa tu ya fedha zinawafanya watu kutengeneza mafundisho ambayo nia yake sio kuujenga ufalme wa MUNGU bali kujinufaisha wenyewe.

Kutokana na kujawa na mafundisho ya utoaji ambayo mengine yamewafanya watu kufilisika vibaya. Baada ya kuambiwa watoe kiasi fulani watapokea mara ndufu, na hawajawahi kuona hicho walichoahidiwa. Wengi tumeumizwa na hili, na kujikuta tumeacha kumtolea Mungu sadaka iliyo safi, akili zetu zikiwa zimevurugwa na wapigaji ambao hawana nia njema.

Kumbe biblia imeweka wazi kabisa utoaji mzuri ambao watu wake waliotoa vizuri, kwa moyo wa kupenda zikaonekana ni sadaka za kumpendeza Mungu mbele zake.

Tunapaswa kuelewa vyote tulivyonavyo ni vya Mungu, pamoja na vyake tunapaswa kutoa kwa ajili ya kazi yake.

Huenda mpaka hapa umeanza kufikiri na mimi nimekuja na silaha hii ya utoaji, ili nikupatie sehemu ya kukupiga pesa yako. Nia yangu sio hiyo ndugu, huenda miongoni mwa watu waliovurugwa katika eneo hili la utoaji nami ni miongoni mwao.

Ila baada ya kusoma maandiko haya kuna kitu kimeugusa moyo wangu sana, kumbe utoaji ni mzuri sana mbele za Bwana ukitoa kwa MOYO WA KUPENDA. Maana wengi wanatoa kwa vitisho vya kuepuka kulaaniwa wasipotoa kiasi fulani alichoambiwa. Badala yake mtu anatoa huku moyo wake unalia kwa sababu haelewi anachofanya ila kutokana na kutishwa, anajikuta anatoa. Huenda ile ile fedha ndio alitegemea kununua chakula au kulipia watoto ada, hapo anakuwa na maumivu mengi,, na ameshindwa kuelewa kwanini alitoa. Maana matokeo ya utoaji wake hujaonekana kama yule mwanamke aliyekutwa na nabii Elia, anaokota kuni za mwisho akapike ale chakula, yeye baada ya kumpikia mtumishi wa MUNGU alipata matokeo mazuri ya utoaji wake.

Hebu naomba ujenge umakini katika hili, natamani upate kitu hapa ili uwe mtu mzuri katika eneo hili la utoaji. Hutatoa kwa sababu unataka watu wakuone, hutatoa kwa sababu unataka mchungaji wako asije akakuona umeasi kwa kuacha kutoa kikumi(asilimia kumi ya mapato/mshahara wako). Utatoa kwa sababu unajua unachotoa kinaenda kufanya kazi ya Mungu, labda kumtunza mtumishi wa MUNGU, au kujenga kanisa au kununua vyombo vya kuhubiri au kwenda kuwaona wajane/yatima au kwenda magerezani.

Nakushauri hili usitoe kwa kigezo cha kutaka baraka, naomba unielewa hapa maana wengi wamepotea kwenye eneo hili. Unapotoa kwanza kabisa jua sehem unayotoa sadaka yako ni sehemu salama, kingine jua hicho unachotoa kinaenda kufanya kazi fulani ya Mungu.

Baraka zipo tu ila nataka unielewe vizuri hapa, uache kukimbizana na upepo wa kuzitafuta baraka wakati zipo miguuni mwako, hujajua tu namna ya kuzichota hizo baraka.

Ninaposema moyo wa kupenda najua unanielewa vizuri, labda niseme hivi utanielewa, kuna mtu anaweza kukuomba pesa usijikie kumpa kabisa. Na kuna mtu anaweza kukuomba pesa ukampa hata bila kuhoji anaenda kuifanyie nini. Unafikiri ni kwanini, huenda aliyekuomba wa kwanza hujui hiyo pesa anaenda kufanyia nini au unamwelewa vizuri akipata pesa anaenda kuitumia vibaya katika matumizi yasiyo sahihi.

Lakini kwa pamoja tukielewa utoaji wetu unalenga nini, na kwa nini tunatoa mali zetu au fedha zetu, tutakuwa na moyo wa furaha sana pindi tutoapo sadaka zetu. Wala hatutafikiria sana maana tunajua tunachofanya, nilikuambia usitoe kwa kigezo cha kubarikiwa. Wewe tayari ni mbarikiwa ndio maana unacho kitu cha kumtolea Bwana aliyekumpa vyote.

Hebu tuone maandiko haya yanaweza kukupa mwanga kwa hiki ninachokisema hapa;

Nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia. Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu.1 NYA. 29:7‭-‬9 SUV.

Jambo la kushangaza sana ujue, kumbe wanaotoa kwa moyo wa kupenda huwa na furaha ndani yao, tena furaha yao ni kuu mno. Inakuwaje sasa unatoa fedha yako lakini moyoni unajisikia huzuni badala ya kufurahi kuwa umemtolea Bwana wako. Sababu ya msingi sana ni umetoa kwa moyo usio wa kupenda, yaani umetoa sehemu ambayo hukuelewa kwanini umetoa.

Kitu kingine cha msingi kwa mtu anayekusisitiza utoaji, lazima na yeye awe mtoaji. Utaona mfalme Daudi alifurahia kitendo cha watu wake kutoa kwa furaha, yeye akiwa mstari wa mbele kuanzisha utoaji huu.

Rejea:Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu; yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba; ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA? 1 NYA. 29:3‭-‬5 SUV.

Umeliona hilo jambo hapo juu, anayekusisitiza utoe tayari yeye alishatoa, sio anayekuambia toa yeye hatoi ila anataka kupokea kwa wengine. Mtumishi wa Mungu Daudi amelionyesha hili kwa uwazi kabisa ndio maana tunaona watu wake waufurahia baada ya utaoaji wao.

Tunaona kitu kingine cha msingi sana, baada ga utoaji ule, mtumishi wa MUNGU Daudi aliomba Mungu juu ya utoaji ule wa watu wake. Akamweleza Mungu sababu ya wao kutoa matoleo yao ya moyo wa kupenda.

Turejee maandiko haya;Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. 1 NYA. 29:16‭-‬17 SUV.

Nimejakupitisha maandiko machache ili upate mwanga mzuri wa utoaji, huenda hapo ulipo ulishakuwa na mtazamo hasi juu ya utoaji. Na uliona haifai tena kutoa fedha zako au mali zako kwa ajili ya Bwana, kwa kuingizwa mjini na wapigaji.

Kuanzia sasa badili mtazamo wako hasi na kuwa na mtazamo chanya juu ya utoaji wako, nakukumbusha tena, elewa sehem unayotoa utoe kwa moyo wa furaha. Usipoelewa utatoa kwa moyo wa maumivu na majuto, ambapo hicho kitu hakitakiwi kabisa.

Mpaka hapo utakuwa umepata kitu cha kukusaidia, usiache kutoa kwa sababu kuna eneo ulivurugwa. Toa kwa moyo wa kupenda na si kutishwa, kwa kufanya hivyo utaona kubarikiwa sana.

Unapenda kuunganishwa katika group la Wasap la kusoma NENO la MUNGU kila siku, unakaribishwa kwa kuwasiliana nasi kwa wasap no +255759808081.

Ndugu yako katika Kristo,
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.