Maandiko yanatuambia kwamba; Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. ISA. 1:18 SUV.

Wekundu wa dhambi yako unaweza ukawafanya watu wakuhukumu na kuona kwamba dhambi yako haiwezi kusamehewa.

Lakini sivyo Mungu anavyomtazama mtu huyo, Mungu anapokuwa kwenye kiti cha enzi anatamani kuona huyo mtu anatubu nakumrudia.

Mungu anapokuwa katika kiti chake cha enzi, anatamani tutubu makosa yetu nakumrudia yeye, hapendi hata mmoja wetu aangamie.

Tunaona mfano kwa mfalme Ahabu baada ya Yezebeli mkewe kumkosesha, alijikuta anamkosea Mungu kwa kuruhusu uovu katika nyumba yake.

Alianza yeye kuingia tamaa kwa habari ya shamba la Nabothi, ndio ndio maana hata Yezebeli alipomuona amehuzunika kwaajili ya lile shamba alipata nafasi yakumchochea akubaliane na mawazo yake maovu.

Lakini Ahabu baada ya Eliya kumletea ujumbe kutoka kwa Bwana aligundua kwamba amekosea na akaingia kwenye toba ya kweli.

27 Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. 1FAL 21:27

Tunaona vile alijidhili mbele za Mungu akaenda kwa upole, inamaana kwamba aliingia kwenye maombi ya toba juu yake.

Lakini pamoja na ile dhambi yake kuwa nyekundu kama bendera, Mungu alizifanya nyeupe, maana alimsamehe uovu wake na dhambi zake.

Rejea: 28 Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,
29 Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.
1FAL 21:28-29

Tunaweza kuona ni jinsi gani Mungu hatazami kama atazamavyo mtu, ndiyo maana tukimwendea kwa unyenyekevu na kutubu anasamehe makosa yetu.

Mungu wetu ni mwingi wa rehema, hahesabu mabaya haijalishi dhambi yako ni ya namna gani, leo hii anatamani akuone ukitubu na kumrudia yeye.

Mungu akubariki sana.
By Rebecca Francis.