“Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane”, Yn 5:5 SUV.
Mtu huyu anayezungumzwa na biblia katika andiko hili, alipitia kipindi kirefu sana cha mateso.
Kipindi ambacho kilijaa kukata tamaa baada ya kutafuta msaada wa Mungu kwa muda mrefu pasipo mafanikio.
Aliendelea kumtumaini Mungu kwa kuamini atamponya na shida yake iliyokuwa inamsumbua katika mwili wake.
Wakati Yesu anamuuliza wataka nikufanyie nini, hakujibu swali hilo alienda moja kwa moja kueleza changamoto aliyokuwa anakutana nayo.
“Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu”, Yn 5:7 SUV.
Kumbe siku yake ya uponyaji ilishafika, Yesu alimhurumia na alimponya na shida yake ngumu iliyomfanya ateseke kwa kipindi chote cha miaka 38.
Nini tunajifunza hapa, somo kubwa la kujifunza hapa ni kutokukata tamaa, yapo mambo mazito tunapitia katika maisha yetu, hatupaswi kukata tamaa.
Yamkini kuna ugonjwa umekusumbua kwa muda mrefu, usiache kumwamini Yesu, saa yako ya uponyaji wako itafika.
Utaona wengine wakiponywa, usijione Mungu amekuacha katika shida yako, mtumaini yeye siku zote za maisha yako.
Inawezekana sio ugonjwa ila kuna tatizo gumu unapitia katika maisha yako, linaweza kuwa la uchumi, au kifamilia, au kikazi, wewe simama katika kumwomba Mungu.
Saa ikifika hutosubiri msaada wa mtu wa kukuingiza kwenye birika la uponyaji, Yesu mwenyewe atakuponya au atakusaidia juu ya shida yako.
Kumbuka miaka 38 inaweza ikawa rahisi kutamka na kusoma ila ukaiona miaka 5 ya kukosa mtoto au kazi au mume au mke ni mingi sana ikakufanya ukakata tamaa kabisa.
Uwe mvumilivu, ukijua yupo aliyepitia kipindi cha miaka 38 akiwa kwenye shida na saa yake ya uzima ilimfikia.
Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081