Unapokuwa na moyo wa kibinadamu, unaweza ukaonywa ukaonyeka, unaweza ukawa na huruma na watu, na unaweza kuwajali wengine kutokana na hali zao.

Moyo wa ubinadamu unapotoka na kuwa na moyo wa mnyama, kufikiri kwako napo kunabadilika, hutakuwa yule tena ambaye anakuwa na utu ndani yake. Kufikiri kwako na kutoa maamzi kwako, inaweza kuleta utata mkubwa sana.

Akili yako inakuwa sio akili ya kibinadamu kabisa, akili yako inakuwa ya mnyama. Hata matendo yako na kufikiri kwako kunakuwa kinyama kinyama tu, yaani unaweza ukawa na akili ya ng’ombe, mbuzi, fisi, mbweha, simba, paka, nk.

Watu wanaweza kushindwa kuelewa vile unaenda, vile unaongea, vile unatoa maamzi, vile unajiweka rafurafu, vile unakuwa mkali, na vile unakuwa na tabia chafu. Kumbe ndani yako una moyo wa mnyama mwenye sifa/tabia kama yako.

Hili tunapaswa kuwa nalo makini sana, hasa pale tunapoanza kujiinua wenyewe, hasa pale tunapoasi, hasa pale unapokuwa na tabia zisizoeleweka. Jiangalie kwa makini sana, ikiwezekana tafuta msaada wa kiroho usaidiwe.

Hili tunajifunza kwa mfalme Nebukadreza, Mungu alimsemesha katika ndoto, kuwa atampa moyo wa mnyama. Maana yake akili yake itakuwa inawaza kinyama nyama, matendo yake yatakuwa ya kinyama nyama.

Kula ya mfalme Nebukadreza, itakuwa ya kinyama nyama, yaani kula majani kwa mfalme Nebukadreza itakuwa kawaida kwake. Ni kama jambo haliwezekani ila unapaswa kuelewa kwa Mungu linawezekana kabisa.

Rejea: Moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake. DAN. 4:16 SUV.

Mungu alitaka kumpitisha mfalme Nebukadreza shule ngumu kwa muda wa miaka saba, baada ya shule hiyo ngumu mfalme Nebukadreza aweze kutambua nafasi ya Mungu. Maana mfalme Nebukadreza alifika mahali akajitengenezea sanamu ya kuchonga ili watu waiabudu.

Tunasoma maandiko matakatifu baada ya miaka saba kupita, miaka ambayo naifananisha kama shule ya mfalme Nebukadreza kujifunza. Fahamu zake zilimrejea na kutambua ukuu wa Mungu, na kukiri kwa kinywa chake mwenyewe.

Rejea: Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi; DAN. 4:34 SUV.

Hapa tunajifunza mambo makubwa sana, wapo watu wanaweza kuleta dharau juu ya Mungu. Mungu hatashindwa kuwapa shule ya mfalme Nebukadreza, ugumu mwingine wa mioyo ya watu ni kwa sababu imefanywa kama ya mnyama.

Mungu atusaidie sana tusiwe na mioyo ya wanyama, tuwe mioyo ya utu, moyo wa kibinadamu. Moyo unaoweza kusikia injili ya Yesu Kristo, moyo unaoweza kusikia Neno la Mungu na ukabadilika na kuziacha njia zake mbaya.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.